Mke amkimbia mumewe na kumuachia mtoto wa miaka mitatu


Na Hamisi Abdulrahmani, Masasi

  MWANAMKE mmoja aliyetambulika kwa jina la Fatuma Salumu ( 38) Mkazi wa kijiji cha Lukuledi wilayani Masasi Mkoani Mtwara,ametoweka nyumbani kwa mume wake, Omari Mtopwa, maarufu Mzee Omari Yanga( 60) na kumuachia mume wake huyo mtoto mdogo wa umri wa miaka mitatu.
  
  Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake Mtaa wa Upanga kata ya Napupa,wilayani Masasi, mume wa mwanamke huyo,Omari Mtopwa mwenye umri zaidi ya miaka 60 alisema tangu mke wake aondoke nyumbani ni siku zaidi ya 15 hajarudi nyumbani na hajulikani aliko.

  Alisema kuwa moja ya shida kubwa anayoipata kwa sasa ni jinsi ya kumlea mtoto huyo ambaye muda mwingi amekuwa akilia na kumlilia mama yake.

  Mtopwa alisema tarehe 24/ 12 / 2019 mke wake,Fatuma aliaga kuondoka nyumbani anakoishi na mume wake mtaa wa Upanga Masasi na kwenda nyumbani kwa wazazi wake kijiji cha Lukuledi kwa ajili ya kwenda kushiriki shughuli za sherehe ya kuwatoa watoto jando.

  Alisema alipoondoka kwenda huko kijijini Lukuledi aliamuacha mtoto wake nyumbani na kuondoka lakini baada ya kuondoka hadi sasa hajarudi tena kwa mume wake licha ya jitihada za kumtafuta kufanyika.

  Mtopwa alisema hadi anaondoka nyumbani siku ya tarehe 24 disemaba mwaka jana hawa jawa na mgogoro wa aina yeyote katika ndoa yao na anashangaa mke wake kufanya kitendo hicho hasa cha kumuachia mtoto mdogo.

  "huyu ni mke wangu wa ndoa na tangu tufunge ndoa yetu sasa ni zaidi ya miaka sita na pia nimezaa mtoto mmoja na ana umri wa miaka ya mitatu lakini hadi anaondoka hapa nyumbani hatuna kabisa ugomvi katika ndoa yetu," alisema Mtopwa 

  Alisema baada ya kuona siku zinazidi kwenda aliamua kufanya mawasiliano na wazazi wa mke wake ambao ni wakwe zake kujua kama alikuwepo kwenye sherehe ya unyago ambayo aliaga kwenda kushiriki kijijini Lukuledi.

  Mtopwa alisema tayari ameshatoa taarifa polisi juu ya kutoweka mke wake na kwenda kusikojulikana na kupewa taarifa ya kipolisi yenye namba, Mass/ RB /2020 iliyofunguliwa tarehe, 6 / 1/ 2020 

   Alisema hivi sasa inakuwa vigumu kwake kutoka nyumba na kwenda kufanya shughuli zake za kumtafuta riziki kwa sababu ya kukaa na mtoto wake ambaye bado  ni mdogo aliyeachiwa na mke wake.

Akizungumzia taarifa hiyo baba mzazi wa mwanamke huyo, Salumu Hamisi alisema ni kweli tarehe 24 disemaba alifika Lukuledi na kushiriki sherehe za unyago zilizofanyika nyumbani kwao Lukuledi.

  Alisema tarehe 29 disemba mwaka jana mwanae aliaga kurudi kwa nyumbani kwa mume wake Mjini Masasi na aliondoka kwa njia ya kukodi usafiri ya bajaji hivyo wao walishafahamu kuwa angekuwa ameshafika kwa mume wake.

  Alisema walishangazwa kupata taarifa kutoka kwa mkwe wao kuwa mtoto wake hajarudi kwa mume wake hadi sasa.

  "Tumejaribu kufanya mawasiliano kwa ndugu na jamaa wote na tumeambiwa hayupo hivyo sisi tunaendelea kumtafuta maeneo mengine ili kuhakikisha tunampata,"alisema Hamisi

  Alisema wao kama wanafamilia hawajafurahishwa na kitendo kilichofanywa na mtoto wao kwani ni jambo la aibu kwao na jamii kwa ujumla.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items