Na Paschal Malulu-Kahama
Mvua za Masika zinazonyesha kwa sasa zinaendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya barabara hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuleta adha ya kuingia maji katika makazi ya Wananchi waishio mabondeni pamoja na kukwamisha shughuli za uchumi.
Hali hiyo imesababisha zaidi ya mifuko 10,000 ya mawe yanayosadikiwa kuwa na Madini ya Dhahabu kukwama na kutotoka nje ya Mgodi huo wa kikundi cha Pamoja Mining Gold Rush Group uliopo kijiji cha Wisolele Namba Sita Kata ya Segese Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Kahama mkoani Shinyanga kwa lengo la kuuza mawe hayo baada ya matajiri kushindwa kufika hapo kutokana na bara bara kuwa mbovu kutokana na mvua hizo.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa sasa Miundombinu ya Bara bara inaendelea kuimarishwa na kampuni ya Tingwa Co.Ltd ya mjini Kahama inayoshughulikia kipande cha barabara ya Ntobo na Segese ambako ndiko kunachangamoto kubwa inayosababisha magari mengi kukwama na kusababisha msululu mkubwa wa magari makubwa kutokana na barabara hazipitiki kutokana na mvua zinazonyesha kwa sasa.
Licha ya Mkandarasi kutoka kampuni ya Tingwa Co.Ltd kushughulikia ubovu wa barabara hiyo lakini hali hiyo imegeuka kuwa shubili kwa Wachimbaji wadogo wa Dhahabu katika mgodi huo ambao wamedhamilia kwa dhati katika kuhakikisha wanaiunga mkono Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kile kidogo wanachokipata licha ya kutokuwa na Leseni ya umiliki wa Mlima wanakochimba Dahahabu.
Imeelezwa kuwa wachimbaji wadogo wa Dhahabu kutoka Kata ya Segese walioungana kwa pamoja na kuunda kikundi cha Pamoja Mining Gold Rush Group kwa sauti moja wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ambapo kwa sasa wamepania kutekeleza miradi mingi katika Kijiji cha Wisolele licha ya kuwepo kwa Rush tatu zinazopata faida baada ya uzalishaji waMadini ya Dhahabu.
Khamis Mabubu ni Mwenyekiti wa kikundi hicho ambapo anasema kuwa Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa Mikoa hapa nchini iliyobarikiwa kuwa na Madini mengi ya Dhahabu huku akisema kuwa licha ya kuwepo kwa makampuni makubwa ya uchimbaji wa Madini hayo pia kuna Rush nyingi ambazo humilikiwa na wachimbaji wadogo wanaovumbua Dhahabu kisha kutimuliwa kama mbwa sehemu waliyovumbua huku wakiitwa wavamizi kwakuwa hawana Leseni ya umilikishwaji wa maeneo yenye Dhahabu.
Mwenyekiti huyo wa Kikundi cha Pamoja Mining Gold Rush Group anasema kuwa kwa sasa anasubili Leseni ya uchimbaji katika eneo hilo huku akijiapiza kwamba kama kikundi ambacho kinajihusisha na shughuli za Uchimbaji wa Dhahabu katika eneo hilo kwa kipindi hiki cha 2020 watahakikisha wamefanya mabadiriko katika kijiji cha Wisolele kwa kuwekeza miradi mingi mikubwa katika Sekta muhimu za Afya, Elimu, Miundombinu na Maji.
Mabubu anasema kuwa Kwa sasa biashara ya Mawe ya Dhahabu imedoda kutokana na ukosefu wa miundombinu Bora ya Barabara inayokwenda katika kijiji cha Wisolele kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha na kukwama kuuza mawe hayo katika sehemu mbalimbali ambapo katika Rush yake zaidi ya Mawe ya Dhahabu 10,000 yameshindikana kuuzwa na hayatoki nje ya eneo hilo kwa jamu ya Barabara.
“Kwa kweli tunamshukuru Rais Magufuli kwa kututhamini sisi Wachimbaji wadogo kwani sisi wenye Rush hizi ndodo ndogo ni wawekezaji wazuri kwenye maeneo yetu ya kijiji na tunatoa gawio kwa serikali ya kijiji ambayo ni 1.5 sawa na mifuko 500 ya mawe hiyo ni kwaajili ya kufanya shughuli za maendeleo kwa wananchi wanaozunguka mgodi,” anasema Khamis Mabubu na kuongeza.
“Tunaitumia fursa ya Rais vizuri kuturuhusu tuendelee na uchimbaji bila kubughudhiwa niwaahidi tu waandishi sisi tutafuata maelekezo ya Serikali na tutafanya shughuli za uchimbaji huo kwa uzalendo mkubwa ili kuinufaisha jamii iliyopo katika kijiji hiki sema kwa sasa kipindi cha mvua za masika mawe hayatoki kwenda Mwazimba, Bukandwe, Nyangarata kutokana na matajiri kushindwa kuleta gari zao kwa kuhofia kuzama,” anasema Khamis Mabubu mwenyekiti wa Mgodi Pamoja Mining Gold Rush Group.
Mabubu anasema kuwa kama watamilikishwa Leseni haraka watafanya mambo makubwa ya uwekezaji kama ilivyo kwa makampuni makubwa yenye mitaji mikubwa kama Mgodi wa Bulyanhulu ulioko Kata ya Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala na Ule wa Buzwagi uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama unaomilikiwa na kampuni ya Twiga.
Anasema kuwa katika mgodi huo kunajumla ya Duara 180 kati ya hizo Duara 80 ndizo zinazozalisha Dhahabu huku akitaja kuwa Licha ya changamoto ya ubovu wa miundombinu inayowatesa tangu mwezi wa 7/2019 Mgodi wa Pamoja Mining Gold Rush Group umetoa kodi ya Serikali kiasi cha shilingi Milioni 23 hadi sasa na kuongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa suala la afya linaboleka kijijini hapa pia Mgodi umetenga kiasi cha shilingi Mil.4 kwaajili ya matundu manne ya choo katika Dhahanati ya kijiji hicho.
Pia anasema kuwa Mgodi umeamua kusimamia Zahanati ya Wisolele ambayo boma lake lina miaka 15 halijakamili lakini baada ya kuanza kazi kwa mgodi huo na hatua za kuikamilisha zikaanza kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji hicho ambapo kwa sasa tayari jingo hilo lililotelekezwa limepauliwa kwa nguvu yao na huku akisema kuwa baada ya zoezi la zahanati Mgodi utajikita katika suala la Elimu kwa kutenga mifuko kadhaa ya mawe ili kuanzisha ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na vyumba vya Madarasa.
“Pamoja na kwamba Rush zingine hazijaguswa na hali ya Wanakijiji lakini mgodi tumeanza kutekeleza mradi wa Zahanati ili kunusuru wanawake wajawazito na wagonjwa wengine kutembea umbali mrefu wa kilomita 10 kwenda kupatiwa matibabu, lakini pia hata wachimbaji wetu itawasaidia pindi wanapopata ajali wakati wakiwa kazini kwani huwa tunateseka kuwapeleka Kahama kilometa kadhaa lakini iwapo Zahanati yetu itakamilika tutaanzia hapa kupata huduma ya kwanza kama itashindikana baadaye tutaenda nje ya wisolele,” anasema Mabubu kwa kupania maendeleo.
Anaiomba Serikali wilayani Kahama kuingilia kati kuwasaidia suala la ujenzi wa miundo mbinu iendayo mgodini iboreshwe ili mawe yanayokwenda kusagwa katika makarasha huko Mwazimba na katika plant njia iweze kupitika ili kuzidi kuleta maendeleo kwa Wananchi huku akisema kuwa kama kiongozi wa mgodi huo atashirikiana na Serikali na ameanza kujikita kujenga barabara ya kwenda Segese ili isaidie wachimbaji wake wanaopata dharula ya kuugua ama kujeruhiwa wakati Zahanati hiyo ikiendelea kukamilika.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Dkt. Ntanwa Kilagwile akizungumza na waandishi wa Habari waliofika ofisini kwake hivi karibuni ili kujua halmashauri inatekeleza kwa kiwango gani ujenzi wa barabara ziendazo katika migodi midogomidogo alisema kuwa Halmashauri inamitambo ya ukarabati wa barabara na hivyo kutumia fursa ya Waandishi wa Habari kuomba uongozi wa mgodi kuandika barua ya kuomba msaada wa mitambo hiyo ili kutatua Changamoto hiyo.
Pia Dkt. Kilagwile alisema kuwa hata hivyo suala la ukarabati wa miundombinu ya barabara jukumu hilo limebaki kwa wakala wa bara bara za Mijini na Vijijini (TARURA) lakini Halmashauri kwakuwa inatambua mchango wa Wachimbaji wadogo itahakikisha inashirikiana nao.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa akizungumza na mwandishi wa Makala haya kwa njia ya simu yake ya kiganjani juu ya changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara kutokana na mvua za masika alikili kuwepo hali hiyo na kumhakikishia mwandishi wa Habari hizi kuwa akikata simu tu atatoa maelekezo kwa watendaji wanaohusika na suala la miundombinu ambao ni Wakala wa Barabara za Barabara nchini TANROADs na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA na sasa tunaona utekelezaji unaendelea nadhani kwa hili la changamoto ya Wisolele litashughulikiwa.