RC ashauri baraza la wafanyakazi kudumisha maelewano mazuri katika sehemu ya kazi

Na Hamisi  Abdulrahmani, Masasi         

BARAZA la wafanyakazi la Sekretarieti Mkoa wa Mtwara limeshauriwa kuongeza nguvu kuhakikisha linadumisha maelewano,ushirikiano na mshikamano kati ya wafanyakazi,uongozi na taasisi husika sehemu ya kazi ili kuweza kuleta tija kwa taifa.

 Ushauri huo ulitolewa jana wilayani Masasi mkoani hapa na mkuu wa mkoa Mtwara,Gelasius Byakanwa alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Baraza la wafanyakazi katika Sekretarieti mkoa wa Mtwara, mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Masasi.

 Byakanwa alisema Baraza la wafanyakazi linawajibu wa kuhakikisha kunakuwepo na ushirikiano, maelewano, mshikamano katika sehemu ya kazi makazini.

  Alisema uwepo wa mshikamano na maelewano katika sehemu ya kazi kwa wafanyakazi kutasaidia kuongeza tija ya utendaji kazi jambo ambalo mwisho wa siku litaleta faida kubwa kwa taifa.

  Byakanwa alisema moja ya siri kubwa katika kuleta mafanikio sehemu ya kazi ni kujenga umoja, mahusiano na maelewano tofauti na hapo hakuna mafanikio yeyote yatakayoletwa na mfanyakazi.

  Alisema hakuna sababu kwa wafanyakazi kufanya kazi kulingana na matabaka yao ya kikazi bali lazima kuwepo na hali ya mshikamano na umoja kwa kila mfanyakazi ili kuwepo na tija.

"Hakikisheni mnadumisha ushirikiano na maelewano kwa wafanyakazi,uongozi na taasisi husika kwani hii itaondoa ufanyajikazi
wa kitaba na kuleta umoja kwa kila mfanyakazi," alisema Byakanwa

  Alisema iwapo kunakuwa na lugha moja ya maelewano kwa wafanyakazi,uongozi na taasisi husika sehemu ya kazi hata migogoro ambayo inayojitokeza baina ya wafanyakazi haitakuwepo kwa sababu wafanyakazi watakuwa kitu kimoja.

  Byakanwa alisema Baraza hilo la wafanyakazi ndiye nyenzo kuu ya wafanyakazi hivyo linalowajibu wa kumtafuta changamoto za wafanyakazi na kuzifanyia kazi ili kujenga ushirikiano kazini.

  Alisema Baraza hilo pia lazima lihakikishe maslahi ya wafanyakazi ikiwemo kupata stahiki zao za upandishwaji wa madaraja wanapata.