Ufilipino: Watu 45,000 wahamishwa kuepuka mlipuko wa volkano

Mamlaka nchini Ufilipino zimewaonya wananchi waliokimbia maeneo yaliyo karibu na mlima wa volkano unaolipuka, kutorejea katika makaazi yao kwa sababu hatari itokanayo na mlima huo itaendelea kuwepo kwa siku kadhaa zijazo.

Mlima huo wa Taal ulio umbali wa kilomita 66 kusini mwa mji mkuu, Manila, umekuwa ukirusha angani lava na jivu la moto kwa siku tatu mfululizo.

Maafisa wamearifu kuwa watu wapatao 45,000 wamezihama nyumba zao, lakini ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na huduma za kibinadamu imetoa tahadhari, ikisema watu takriban 460,000 walio katika eneo la kilomita 14 linalozunguka Mlima Taal, wanaweza pia kuathirika.

Volkano ya Taal iliripuka mara ya mwisho mwaka 1977, lakini imekuwa mnamo miaka ya 2008, 2011 na 2019 ikionyesha dalili za kukaribia kuripuka tena.