Waajiriwa kwa ajili ya Uandikishaji wapiga kura wapya watakiwa kufuata kanuni na Sheria - ZEC



Na Thabit Madai,Zanzibar.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Imewataa watendaji wa Tume hiyo walioajiriwa kwa ajili ya Uandikishaji wa wapigakura wapya na uhakiki wa Daftari la kudumu la wapiga kura kufanyakazi zao kwa kufauata kanuni na sheria za Tume hiyo  ili kumuwezesha kila mwenye sifa kupata haki yake.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina, katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Madungu Chake chake Pemba , wakati akifunguwa mafunzo kwa  Wakuu wa vituo na Makarani wa Uandikishaji wapiga kura wapya na wahakiki wa taarifa za wapigakura wa Kisiwa cha Pemba ikiwa ni matayarisho ya zoezi hilo linalotarajiwa kuanza rasmi tarehe 18 mwezi huu katika Wilaya ya Micheweni Kisiwani humo.

Alisema  Tume hiyo imejipanga na itaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizowekwa ili kuufanya Uchaguzi mkuu  unao kuja wa mwaka 2020 kuwa huru na haki na kuhakikisha kila mwenye sifa ya kuwa mpigakura anatekeleza haki yake.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Tume  ya Uchaguzi (ZEC) imeandaa maelekezo kwa mamlaka iliyonayo chini ya kifungu cha 142 cha Sheria ya Uchaguzi  ya mwaka 2018 na kutowa muongozo kwa Makarani wa Uandikishaji katika utendaji wa kazi zao ndani ya Vituo.

Kwa upande wake mkuu wa Kurugenzi ya IT kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mwanakombo Machano Abuu,aliwataka Wananchi kuhakikisha kila atakae kwenda kuandikishwa katika Daftari la kudumu lazima aende na Kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi kipya na akioneshe kwa muhusika wa kituo.

Alisema pamoja na hilo lazima atekeleze matakwa ya kisheria kwa kuwa na umri usiopunguwa miaka 18 na mkaazi wa eneo husika sio chini ya miezi 36 hapo ndipo atakuwa na haki ya kuandikishwa katika Daftari la kudumu ili kuweza kutumia Demokrasia yake ya Uchaguzi unaokuja.

Hivyo Watendaji hao wametakiwa kuelewa kuwa zoezi la Uandikishaji litaanza kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa kujibu wa ratiba ya Uandikishaji na kabla ya kufunguwa kituo , karani wa Uandikishaji anatakiwa kutowa maelekezo kwa Mawakala waliopo juu ya utekelezaji wa kazi Kituoni.