Bwege asema hata serikali ikijenga barabara za lami hadi uani kwake hawezi kwenda CCM. 

Na Ahmad Mmow, Lindi. Mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini,Seleman Bungara( Bwege) amesema kwa jinsi asivyokipenda Chama Cha Mapinduzi (CCM) na asivyopenda kuwasaliti wananchi waliomchagua, hawezi kujiunga na chama hicho hata kama serikali itajenga barabara za kiwango cha lami nakufikisha hadi ndani ya nyumba zake.

 Bwege ameyasema hayo leo kutoka Kilwa Kivinje, baada ya kuombwa na Muungwana Blog aeleze msimamo wake na hatima yake kisiasa kufuatia wabunge wa wananchi kupitia vyama vya upinzani kuhamia CCM.

 Alisema ni jambo lisilowezekana ajiunge na CCM wakati maisha yake na yawananchi anaowawakilisha ni magumu. Kwamadai kwamba ugumu huo wa maisha umesababishwa na chama hicho kikongwe miongoni mwa vyama vikongwe barani Afrika.
Alisema wanaodhani mafanikio madogo yanayoonekana ni makubwa wanajidanganya. Kwani juhudi zao hazilingani na mafanikio waliyonayo na hata umri wa Uhuru wa Tanganyika haulingani na maendeleo yaliyopatikana.

 " Mafanikio niliyonayo mimi na hata wewe( mwandishi wa habari hii) yangekuwa makubwa zaidi hata mara kumi ya sasa. Lakini hao ndio walifubaza maendeleo yetu, siwezi kujiunga na CCM hata kama ikifikisha lami hadi ndani ya uwa za nyumba zangu.

Sijiungi na CCM ng'ooo," Bwege alisisitiza. Mbali na sababu hiyo, mbunge huyo alitaja sababu nyingine inayomfanya asifikirie kujiunga na CCM nikutopenda kuwasaliti wananchi waliompigia kura na kumchagua awe mbunge wao.

Kwani wapo walio umia, kupata ulemavu wa viungo na kupoteza mali zao kwa ajili yake. Alisema kinachofanywa na wabunge waliohamia CCM kutoka upinzani ni usaliti na ukatili mkubwa dhidi ya wananchi waliowachagua.

Kwamadai kwamba kutangazwa wagombea wa upinzani kama wameshinda kunatokana na nguvu za wananchi ambao wanakuwa tayari kujitoa mhanga il wasimamizi wa uchaguzi wawatangaze.

 " Sasa baada ya kushinda na kuonekana, CCM wale wale ambao walikuwa wanafanya fitina tusitangazwe ndio wanawaona wazuri na kuwasaliti waliowafikisha na kuwafanya waonekane.

Hiyo ni dhambi na ukatili mkubwa," Bwege alisema kwa sauti kali na msisitizo. Mbunge huyo alikwenda mbali kwa kusema wakati wa uchaguzi ni afadhali wananchi wawachague wagombea wa CCM ambao hawakutoka vyama vya upinzani kuliko wahamiaji.

Kwani hawaaminiki na wakatili kwao. Alisema kama CCM kikiwasimamisha wagombea wahamiaji kutoka vyama vya upinzani, basi bora wawachague wagombea wa upinzani.

Kwani kwa mazingira ya siasa ya sasa watakuwa ni watu jasiri wenye nia thabiti ya kuwatumikia. Mwisho.