Msafara wa kijinsia unaolenga kutokomeza vitendo vya kikatili wazinduliwa Katavi

Msafara wa kijinsia unaolenga kutokomeza vitendo vya kikatili kuelelekea Siku ya Wanawake Duniani umezinduliwa rasmi mkoani Katavi.

Akizungumza wakati akizindua Msafara huo Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Juma Zuberi Homera amesema kuwa vitendo vya kikatili vimekuwa vikishamiri kila siku katika jamii zetu hivyo vinatakiwa kupatiwa mbinu ya kupambana navyo.

Ameongeza kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona wanawake na watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili hivyo itahakikisha inazishugulikia kesi zote za vitendo vya ukatili.

“Sheria ifuate mkondo hata mimi naweza kutelekezwa na hata mimi nikitelekeza nikamatwe tu” alisema

Mhe. Homera amesisitiza vyombo vya Sheria na Taasisi zisizo za Kiserikali kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanapata mbinu stahiki itakayosaidia kuondokana na vitendo vya ukatili.

Akizumgumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Bi. Imelda Kamugisha amesema lengo la msafara huo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili na namna ya kupambana na vitendo hivyo kuelekea maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani.

“Msafara huu umelenga kutoa elimu kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili kuendeleza jitihada za Serikali na wadau katika kuhakikisha tunaondokana na vitendo vya kikatili” alisema
Naye Nurdin Bilal Maarufu Shetta amesema wasanii wameungana na Serikali katika kusambaza elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili ili kuwezesha kuondokana na vitendo hivyo kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2025.

“Tuko tayari na tumeamua wasanii kuingia katika haya mapambano muhimu ya kitaifa dhidi ya vitendo vya kikatili” alisema.