Shirika moja la habari nchini Haiti limeripoti kuwa mtu mmoja amefariki na wengine wengi wamejeruhiwa baada ya maandamano ya polisi ya kulalamikia kuhusu mazingira ya kufanya kazi, yaliyogeuka na kuwa vurugu.
Sherehe za kanivali katika mji mkuu wa nchi hiyo Port -au-Prince zimefutwa kuepusha ''Umwagikaji damu''
Polisi walifyetuliana risasi na wanajeshi kwa saa kadhaa baada ya maandamano yao kusimama karibu na ikulu ya kitaifa, haikubainika wazi ni upande gani ulioanzisha vurugu hizo.
Mamia ya wananachi walijiunga na polisi kuwaunga mkono.Takriban maafisa watatu wa polisi walijeruhiwa katika mashambulizi hayo ambayo wizara ya ulinzi inasema yalitekelezwa na washambuliaji waliokuwa wamevalia vinyago.
Kwa miezi kadhaa sasa, polisi nchini Haiti wametaka kuimarishwa kwa mazingira yao ya kazi ikiwa ni pamoja na haki ya kuunda chama chao kitakachoweza kuwasaidia katika masuala ya uwazi pale litakapohusika suala la kushughulikia madaraka ya polisi.
Siku ya Jumamosi, rais wa Haiti Jovenel Moise alijaribu kupunguza taharuki iliyokuweko kwa kupendekeza mikakati inayojumuisha kuundwa hazina ya fidia kwa familia za maafisa wa polisi wanaouawa wakiwa kazini pamoja na kuwakatia bima maafisa hao.
