Simba na Mtibwa kuonyeshana ubabe leo


Timu hizo zinakutana leo zote zikitoka kujeruhiwa kwenye mechi zilizopita ambapo Simba ilikubali kipigo cha pili msimu huu kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania huku Mtibwa Sugar nayo ikiwa katika Uwanja wa Gairo ikikubali kipigo kama walichopokea vinara hao wa Ligi Kuu kutoka kwa Lipuli FC.

Mchezo wa leo utakuwa ni wa kila timu kutaka kupooza machungu ya majeraha yake, lakini mechi hiyo itakuwa na sura tofauti kwani Simba watataka kuendeleza rekodi yao ya kuifunga Mtibwa Sugar kufuatia ushindi wao wa mabao 2-1 walioupata mzunguko wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Wakati Mtibwa Sugar yenyewe ikishuka dimbani na ari kubwa ya kutaka kuendeleza kipigo cha bao 1-0 walichoiadhibu Simba kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

Hata hivyo, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila ameliambia Nipashe jana kuwa wameweka kando matokeo ya Kombe la Mapinduzi kwa kuwa mechi ya ligi ni tofauti kabisa na mashindano hayo.

Katwila alisema kwa ujumla kikosi chake hakina majeruhi na kwamba kinampa uwanja mpana wa kukipanga kuelekea mechi hiyo hasa ukizingatia mechi zinachezwa karibu karibu sana.

Alisema wanaingia uwanjani kwa lengo la kusaka pointi tatu kama ambavyo yatakuwa malengo ya Simba, hivyo kiufundi tayari amekiandaa kikosi chake kupambana kupata matokeo mazuri.

"Unajua tatizo mechi zinachezwa 'back to back' hakuna muda wa kupumzika, unacheza leo, kesho unasafiri kisha siku inayofuata unacheza tena, ila tumejipanga na sina majeruhi, kitakachofuata labda 'rotation' ya wachezaji tu," alisema.

Kwa upande wa Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema lengo lao ni kurejesha furaha kwa mashabiki wa Simba baada ya kupoteza mechi iliyopita.

Alisema wamewasili mjini Morogoro tangu juzi saa saba mchana wakiwa na kikosi cha wachezaji 25 pamoja na benchi zima la ufundi na wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi hiyo ambayo alisema itakuwa ngumu kwa kila upande.

"Tunajua mashabiki wetu walihuzunika kutokana na matokeo ya mechi iliyopita, tunaahidi kuwapa furaha na tunaomba waendelee kuisapoti timu," alisema meneja huyo.

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 50 wakati Mtibwa Sugar yenye alama 23 ikiwa nafasi ya 13 baada ya timu hizo kila moja kushuka dimbani mara 20.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia