Stand United yajigamba kuimaliza Simba leo

Kocha Mkuu wa Stand United, Ramadhan Juma amesema kuwa timu yake imejipanga kutikisa nchi hii leo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba leo, Februari 25.

Mchezo huo unatarajia kupigwa katika dimba la Kambarage Mjini Shinyanga, ambapo timu hizo zitapigania nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Kocha Ramadhani amesema kuwa wanaiheshimu Simba kutokana na ubora wao msimu huu lakini wao wamejipanga zaidi kupata matokeo katika mchezo huo, "tunawaahidi mashabiki wa Stand United na Watanzania kwa ujumla kuwa leo tunaitikisa nchi kwa kuichapa Simba", amesema.

"Simba lazima ataacha pointi tatu leo nawahakikishia. Hao kina Kahata, Shiboub na Miquissone ni wachezaji wa kawaida tu kama wakwetu", ameongeza.

Stand United inashiriki katika Ligi Daraja la Kwanza baada ya kushuka kutoka Ligi Kuu msimu uliopita, ambapo sasa inakamata nafasi ya 10 katika kundi B. Mechi zingine za leo Kombe la Shirikisho ni Mbeya City Vs Namungo FC, Panama FC Vs Sahare All Stars, Ndanda FC Vs Kitayosa FC, Ihefu FC Vs Azam FC, JKT Tanzania Vs Alliance FC, Yanga SC Vs Gwambina FC na Kagera Sugar Vs KMC.