Ujerumani: Maelfu waandamana kupinga ubaguzi

Maelfu ya watu wameandamana kwenye mji wa Hanau, Ujerumani kupinga ubaguzi pamoja na makundi ya siasa kali za kizalendo, ikiwa ni siku tatu baada ya mtu anayehusishwa na chuki dhidi ya wageni kuwashambulia na kuwaua watu 11 kwenye mji huo, akiwemo yeye mwenyewe.

Polisi imeripoti kuwa watu wapatao 3,000 walishiriki katika maandamano hayo yaliyofanyika jana Jumamosi kwenye mji huo ulio umbali wa kilomita 25 mashariki mwa Frankfurt.

Baada ya maandamano hayo, mashada ya maua yaliwekwa kwenye eneo ambako mashambulizi hayo yalifanyika usiku wa Jumatano.

Waandamanaji walibeba mabango yenye ujumbe unaosema ''tuungane kupinga ubaguzi na ufashisti'' na ambayo yanakikosoa chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia, AfD kutokana na sera yake ya kuwapinga wahamiaji.

Baadhi ya waandamanaji walibeba picha za wahanga wa mashambulizi hayo mawili yaliyotokea kwenye baa ambako zinavutwa shisha pamoja na mgahawa.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items