UWT yawataka wanawake kutoka mafichoni



Na James Timber, Mara.

Wanawake Mkoa wa Mara wametakiwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu kwa lengo la kutoa mchango wao wa maendeleo chanya katika jamii.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa UWT (CCM) Taifa, Bi Gaudencia Kabaka katika kikao cha Baraza la Wanawake UWT mkoani Mara, ambapo amesema wanawake wamekuwa wakijihisi hawawezi kuongoza na hivyo kuwafanya wasijitokeze kwa wingi kama ilivyo kwa wanaume na hivyo amesisitiza waondokane na dhana ya fikra hasi kuwa hawana uwezo.


"Kule vyuo vikuu sijaona msichana kutoka mkoa wetu anashika uongozi katika nafasi za juu, kutoka kwenye chama chetu cha CCM, niwaombeni wakina mama kuamka sasa na kujitambuà kwamba ni nguzo ya mafanikio katika maebdeleo yoyote yale na wanahaki sawa ya kugombea iwe ni nafasi ya udiwani, ubunge na nafasi zingine ndani ya chama katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa wananchi," amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu kupitia UWT Taifa, Amina Makilagi katika taarifa yake imeeleza kwamba ameweza kushiriki katika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutafuta wahisani ambao wametoa mitaji kwa vijana kutoka vyama mbalimbali ili wajiajiri katika kujikwamua kiuchumi.

Aidha Makilagi, amesema kuwa hivi sasa mafunzo kwa wajasiriamali yanaendelea kutolewa chini ya usimsmizi wake na kwamba kila mhitimu atakapomaliza mafunzo hayo atapewa mtaji wa kuanzia ili kufikia malengo ya kila mmoja alikusudia kuyafikia kiuchumi.