Virusi vya Corona: Wafanyakazi wa afya 1,716 China waambukizwa

Maafisa wa afya nchini China wamesema wafanyakazi sita wa afya wamefariki kutokana na kirusi cha Corona nchini humo, huku zaidi ya 1,700 wakiambukizwa.

Naibu Waziri wa Afya, Zeng Yixin, amesema wafanyakazi wa afya 1,716 wameambukizwa kuanzia siku ya Jumanne.

Wengine 1,102, wamegundulika kuwa na ugonjwa wa COVID-19 unaotokana na virusi vya Corona mjini Wuhan eneo kulikoanzia mripuko huo wa virusi hivyo, huku wengine 400 wakiwa wameambukizwa katika mkoa wa Huabei.

Taarifa ya idadi hiyo ya wahudumu wa afya kufariki wakiwa kazini inaangazia hatari ambayo inawakabili madaktari na wauguzi kufuatia uhaba wa vifaa vya kujikingia.

Idadi hiyo imetangazwa ikiwa ni wiki moja tu tangu raia kuonesha hasira zao kwa mamlaka za taifa hilo kutokana na kifo cha daktari aliyegundua virusi hivyo lakini akazuiliwa na kunyamazishwa na polisi mwezi Desemba.

Serikali ya China inajizatiti kuweka vifaa zaidi vya kujikinga na virusi hivyo katika hospitali zote mjini Wuhan ambako madaktari wamezidiwa nguvu na idadi kubwa ya watu walioambukizwa.