Vulu akabidhi vifaa tiba Mlandizi



Na Omary Mngindo, Mlandizi

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynab Vulu, amekabidhi vifaa tiba katika zahanati za Kikongo na Disunyara, lengo ni kuwapunguzia changamoto wagonjwa wanaopatiwa tiba kwenye zahanati hizo.

Mbali ya vifaa kwenye zahanati hizo, pia Vulu amekitembelea kikundi cha Umoja ni Nguvu kilichopo Kikongo, ambacho amekikabidhi cherehani moja na jora la kitambaa kitachotumika kuwashonea sketi na kaptura wanafunzi 70 wanaoishi kwenye mazingira hatarishi wakisaidiwa na kikundi hicho.

Akizungumza kwenye zahanati ya Kikongo kabla ya kukabidhi mashuka, vipomo vya presha, sukari, apron za kuvaa kifuani na mipira ya kitanda ya kuzuia shuka zisichafuke, Vulu alisema kuwa kwa uchache wake ameamua kufika hapo kukabidhi vifaa tiba hivyo.

Akiambatana na mwenyeji wake Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT)  wilayani hapa Leyla Humoud na Diwani wa Kata Fatma Ngozi, Vulu amesema kubwa amegushwa na changamoto hizo na kufika kuwakabidhi ili kupunguza upungufu uliopo.

"Hapa Kikongo si mgeni, nilishakuja kukabidhi tenki hili la maji, ninafuraha kuliona bado liko vizuri na linatumika, leo nawakabidhi vifaa hivi vichache ambavyo nina imani vitatusaidia katika kuwapatia huduma wananchi wetu wataofika kwa ajili ya matibabu," alisema Vulu.

Akiwa kwenye zahanati ya Kitongoji cha Kilangalanga pia amekabidhi vifaa kama hivyo, ambapo mganga Mkuu wa zahanati hiyo Raya Mohamed na msaidizi wake walifurahia hatua hiyo, huku wakisema kuwa vipimo vya presha na Kisukari vimeharibika hivyo kukabiliwa na changamoto hiyo.

Kwa upande wao madiwani Fatma Ngozi wa Kikongo na Mwajuma Denge wa Kilangalanga walielezea furaha yao ya upatikanaji wa vifaa hivyo, huku wakieleza kwamba vitatumika kama malengo yalivyokusudiwa, na kuwa wanamshukuru Mbunge huyo kwa ushirikiano wake.

Akizungumza na wanakikundi wa Umoja ni Nguvu kabla ya kuwakabidhi cherehani na jora la kitambaa, Vulu alisema kwamba amefika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Humoud Jumaa, alipokuwa kwenye hafla ya kumaliza mzunguko wa mwaka, ambapo alitoa ahadi za wabunge watatu wa Viti Maalumu.

"Nimshukuru kaka yangu Jumaa kwa kuweza kutukutanisha, tukiwa bungeni jijini Dodoma aliniambia kwamba amefika hapa na kutuwekea ahadi ya sisi wabunge watatu kufika hapa kuwaunga mkono kwenye maendeleo ya kikundi chenu," alisema Vulu.

Kwa upande wake Leyla alimshukuru Mbunge huyo, huku akiahidi nae kuumga mkono kuchaangua nyuzi, sindano, mkasi na tepu ya kumpimia mtu anayetaka kushinewa nguo.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items