Waziri Bashungwa awapa neno wadau wa viwanda na biashara

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amewataka
wadau wa Viwanda na Biashara kuendelea kuunga mkono Serikali ya
awamu ya tano kwa kuendelea kutoa ajira katika viwanda vidogo na
vikubwa ili kupunguza adha ya ukosefu wa ajira kwa vijana Nchini.

Ameyasema hayo leo Jumatano katika mwendelezo wa ziara yake ya
kutembelea Viwanda vilivyopo Jijini Dar es salaam na kutoa rai kwa
kwa watanzania kutumia bidhaa zinazotokana na viwanda vya ndani ili
kuongeza ajira kwa vijana

“Hongereni kwa kumuunga mkono Rais wetu Magufuli kwa kuwapa ajira
watanzania 150, ambao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali hapa nchini,
lakini hata wale walikuwa nyumbani wamekaa bila kazi” alisema Mhe.
Bashungwa

Katika Ziara hiyo Mhe. Bashungwa amewapongeza Bwana Charles
Mlawa na Aloyce Ngowi ambao ni wamiliki wazawa wa kiwanda cha
Tropical kilichopo Jijini Dar es Salaam kinachozalisha Vifaa vya Umeme
(Soketi na Transfoma) hapa Nchini kwa lengo la kuunga mkono Serikali
kufikia Uchumi wa kati wenye viwanda.

“Nyie ni wazalendo, ni mfano tosha kwa wawekezaji wazawa kwa
kufahamu umuhimu wa Serikali kufikia uchumi wa kati, transfoma na
nyanya za kupitishia umeme zote zenye ubora sasa zinatengenezwa
Tanzania tena mwenge, Dar es Salaam, na sio tena kuagiza kutoka nje
ya Nchi” alisema Mhe. Bashungwa

Aidha Mhe. Bashungwa alitoa rai kwa wananchi na wadau wa sekta ya
Viwanda na Biashara kuendelea kuunga mkono kwa kununua bidhaa za
ndani zinazo tengenezwa na wawekezaji wazawa na wazalendo.

“Niwaombe watanzania kuendelea kuipa kipaumbele neno ‘MADE IN
TANZANIA’ utajisikiaje umeenda Nchi za watu ukakuta chombo
unachotumia kimewekwa nembo ya Tanzania, hakika ni fahari sana”
alisema Mhe. Bashungwa

Naye Mkurugunzi Mkuu wa kiwanda cha Tropical, Ndugu Charles Mlawa
ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwaunga mkono na
kuwajali katika kuhakikisha sera na lengo la kufikia uchumi wa kati

Nchini ifikapo 2025, kwani mpaka sasa kiwanda hicho kinapata umeme
wa uhakika kutoka Tanesco.

“Nampongeza sana Rais Magufuli kwa kuendelea kutuunga mkono sisi
wawekezaji wa ndani, kwetu sisi ni fahari na tutaendelea kuiunga
mkono Serikali yetu” alisema Bwan. Mlawa

Waziri Bashungwa katika ziara yake, pia alitembelea kiwanda cha
AFRICAB kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam kinacho jihusisha na
utenegezaji wa vifaa vya umeme vya majumbani, kinachomilikiwa na
Wageni kutoka India.