Nchi za Kiafrika zachukua hatua dhidi ya virusi vya corona

Nchi nne za Kiafrika zinazokabiliwa na mripuko wa virusi vya corona, hapo jana zilitangaza hali ya dharura na nafuu ya kodi, katika juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Mali ilichukua hatua hiyo baada ya raia wake wawili waliorejea kutoka Ufaransa kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Libya, ambayo kama ilivyo Mali inakumbwa na mzozo wa kisiasa wa muda mrefu, pamoja na Guinea Bissau, zilithibitisha visa vya kwanza vya virusi hivyo hatari.

Idadi jumla ya maabukizi ya virusi vya corona barani Afrika hapo jana ilifika watu 2,400, huku 64 miongoni mwa waathirika hao wakiwa wameaga dunia, kulingana na takwimu za shirika la habari la AFP.

Ingawa bado kuenea kwa virusi hivyo barani Afrika bado ni kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na Asia, Ulaya na Amerika, wataalmu wa Afya wanasema yumkini kiwango cha maambukizi ni kikubwa zaidi kuliko inavyojulikana, na kitisho kwa bara hilo nim kikubwa.