Ndejembi amuagiza Mhandisi wa Wilaya kumchukulia hatua mkandarasi mradi wa maji Mihingo

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi amemuagiza Mhandisi wa Maji wilaya kuanza kumkata kiasi cha fedha anachodai za siku 100 mkandarasi anaejenga mradi wa maji wa kijiji cha Mihingo.

Mradi huo unagharimu kiasi cha Sh Milioni 600 unajengwa na serikali katika kumaliza changamoto ya maji kijijini hapo lakini pia ukienda na sera ya Rais Magufuli ya kumtua ndoo mama kichwani lakini mpaka sasa umekua ukisuasua.

Baada ya kufika katika mradi huo na kujionea maendeleo yake DC Ndejembi ameeleza kutofurahishwa kwake na kasi ya ujenzi wake licha ya mkandarasi kuongezea muda mara kadhaa lakini bado ameshindwa kumaliza kwa wakati.

" Huu ni uzembe haiwezekani mkandarasi licha ya kuongezewa muda mara kadhaa bado ameshindwa kumaliza katika muda uliokua umepangwa awali, hivyo nakuagiza injinia wa maji wilaya umkate liquidated damage za siku 100 ili tuangalie kama atashindwa basi tuvunje nae mkataba.

Ninampa wiki moja ya kuniletea maelezo ya kwanini hii kazi mpaka sasa hajaimaliza, pamoja na maelezo yake lakini kazi nataka iendelee na mimi Ijumaa nitakuja tena hapa kukagua maendeleo ya ujenzi huu na asipokua na maelezo ya kuridhisha basi nitamchukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kumuachisha hii kazi na kumpa mtu mwingine mwenye kuweza kuifanya kwa spidi na ubora," Amesema DC Ndejembi.

Pia amewataka wakandarasi wote ambao wamepewa miradi mbalimbali wilayani Kongwa kufanya kazi kwa maelekezo ambayo wamepewa na serikali na kwamba hatokua na huruma na mkandarasi yoyote ambaye atashindwa kumaliza kazi yake katika muda aliopangiwa.