Serikali yajivunia viwango vya utabiri TMA

KILA ifikapo tarehe 23 Machi, ya kila mwaka Jumuiya ya
kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa
Duniani. Siku hii ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO), lililoanzishwa mwezi Machi 23, 1950.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa WMO, mbayo imeendelea
kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa kwa kuhakikisha
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) inatoa huduma
za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa.

Utekelezaji huo ni pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya
Hali ya Hewa kwa upande wa vifaa na wataalam ili kuhakikisha wanafuatilia
mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika
nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote ikiwa ni pamoja na
sekta ya maji.

Mwaka jana, 2019, Serikali ilipitisha sheria ya kuhuisha
Wakala wa Hali ya Hewa nchini kuwa Mamlaka kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya
Hewa Na. 2 ya 2019. Sheria hii inaiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake
kitaifa, kikanda na kimataifa na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii ambazo
zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na
tabianchi.

Sheria iliyounda Mamlaka ya Hali ya Hewa inaipa nguvu za
kisheria za kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini na kukusanya mapato
yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara. Pi
sheria hiyo inaitambua Serikali kama mdau mkubwa wa huduma zinazotolewa kwa
matumizi ya wananchi (Public Good) hususan tahadhari za hali mbaya ya hewa.

Kwa mabadiliko na maboresho hayo, Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania inatarajiwa kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini, hivyo
sheria hii imehakikisha uwakilishi, ushirikishwaji, mabadiliko ya kimtazamo na
uwajibikaji wa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na jumuiya za
kijamii.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati) akizinduwa rasmi Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), wengine ni wageni meza kuu katika hafla hiyo.
Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb) ni Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, wizara inayoisimamia TMA, akitoa ujumbe wa Maadhimisho
ya Siku ya Hali ya Hewa duniani mwaka huu, anabainisha kuwa ili kuhakikisha taasisi
hiyo muhimu inatekeleza majukumu yake kiufanisi na kuchangia maendeleo ya
kiuchumi na kijamii nchini.

Serikali inaendelea kuijengea uwezo mamlaka ili iweze
kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa
lengo la kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mfupi na muda mrefu.
Anasema taarifa za hali ya hewa ni muhimu sana katika kutoa maamuzi na kuweka
mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Anasema Serikali inatambua kuwa huduma za hali ya hewa
husaidia na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya
hewa na vilevile kuchangia katika maendeleo endelevu. Hivyo, kuliandaa taifa
vizuri katika kukabiliana na maafa yanayosababishwa na vipindi vya ongezeko au
upungufu wa maji kama vile mafuriko na ukame.

Waziri Kamwele anaongeza kuwa huduma za hali ya hewa
zitolewazo husaidia watumiaji wa huduma hizo kupanga vyema shughuli zao ambazo
ni pamoja na mipango ya utoaji wa huduma za maji mijini, kilimo, mifugo,
maendeleo ya uvuvi, uzalishaji wa nishati na uratibu wa maafa miongoni mwa
sekta nyingine.

“…Serikali inaendelea kuongeza uwezo wa TMA kufuatilia na
kupima hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi katika
sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya maamuzi ya mipango
ya maendeleo katika sekta hizo.”
“Kwa kuzingatia hatua kubwa ya maendeleo iliyopigwa
katika nyanja ya teknolojia na mahitaji yake katika sayansi ya hali ya hewa,
Serikali inaipongeza TMA kwa kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia
katika kuboresha huduma wanazotoa hapa nchini.” Anafafanua Mhandisi Isack Kamwelwe.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (kushoto) akitoa utabiri wa  mwelekeo wa mvua za vuli, kwenye moja ya mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa.

Aidha tangu kuingia kwa Serikali inayoongozwa na
Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, TMA imeboresha zaidi utendaji wa
kazi zake. Hii ni pamoja na utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, hasa baada
ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kivifaa vya kisasa hususani katika
kuboresha miundombinu.

Uwekezaji huu ni pamoja na ununuzi wa Rada za hali ya
hewa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini. Rada
hizo zimefungwa Mwanza na Dar es Salaam na zingine tatu ziko katika hatua ya
ununuzi ambazo zitafungwa  Mtwara, Mbeya
na Kigoma.

Waziri aanasema Serikali itaendelea kuwekeza ili
kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na maji kwa kuongeza uwezo wa
wataalamu na miundombinu huku tukihimiza ushirikiano baina ya sekta mbalimbali
zinazohusiana na zinazotumia huduma za hali ya hewa na rasilimali maji kwa
lengo la kuendelea kuboresha maisha na ustawi wa jamii.
Hata hivyo anashauri jamii kuongeza kasi ya utumiaji wa
huduma za hali ya hewa katika mipango yao na ile ya sekta zote za kiuchumi. Utekelezaji
wa miradi ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu, uendelezaji na uzalishaji
wa nishati inayotokana na maji, kilimo na rasilimali maji.

Nashauri pia tuendelee kuunga mkono juhudi za TMA katika
utekelezaji wa majukumu yao na kuwapa ushirikiano ikiwa pamoja na kuhakikisha
wote wenye vituo vya hali ya hewa vinasajiliwa na TMA ili kwenda sambamba na
matakwa ya sheria.
Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa
Duniani Machi, 23, 2020 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) Dkt. Agnes Kijazi anasema Ipo mifano halisi ya matukio ya hali mbaya ya
hewa yaliyotokea nchini kwa mwaka 2019 na kuathiri upatikanaji na ubora wa maji
katika baadhi ya maeneo.
Matukio
hayo ni pamoja na kuchelewa kuanza kwa mvua za msimu wa Machi hadi Mei
(masika), na matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika msimu huo ambapo
mwezi Mei 2019 ulikuwa ni mwezi wenye mvua nyingi zaidi ya kawaida.


Moja ya rada zinazotumiwa na TMA kurahisisha kazi zake.
 Dkt. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, anaongeza
kuwa matukio ya vimbunga Keneth na Idai katika msimu wa masika 2019, yamesababisha
athari katika maeneo mbali mbali ya nchi ni miongoni mwa changamoto za
mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Kwa msimu wa mvua za mwezi Oktoba hadi
Disemba (vuli) 2019 kumekuwa na mvua nyingi zaidi katika miezi ya Oktoba na
Desemba.

“…Katika mwaka 2020 tumeshuhudia matukio ya mafuriko ya
kutisha katika maeneo mbalimbali ya nchi hususan mkoani Lindi ambayo
yalisababisha athari katika sekta mbali mbali ikiwa pamoja na sekta ya maji. Inatazamiwa
kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame
yataongezeka kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha
athari katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati,
usafirishaji na kilimo,” anaeleza nguli huyo wa masuala ya Hali ya Hewa ulimwenguni.

Pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na
tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji,
taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za
kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji.
Taarifa hizo ni pamoja na data za hali ya hewa za kipindi
kirefu (klaimatolojia), utabiri wa hali ya hewa na matazamio ya mabadiliko ya
hali ya hewa (climate change projections).
Anabainisha kuwa TMA imeendelea kupata mafanikio katika
kutekeleza mpango mkakati wake, ikiwa ni pamoja kuendelea kumiliki cheti cha
ubora wa huduma kutoka Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification)
katika huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.

Kwenye mafanikio changamoto hazikosekani. Kwa sasa
changamoto ni uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya
matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya taarifa za
sekta maalumu na maeneo madogo madogo na athari za mabadiliko ya hali ya hewa
na tabianchi katika misimu ya mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya
hali mbaya ya hewa.

Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka
2020, anatoa wito kwa wadau wa huduma za hali ya hewa kutoka sekta zote za
kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia ipasavyo huduma za
hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi nchini.