Viongozi wa ulimwengu waapa kupambana na COVID-19


Viongozi kutoka kundi la nchi zenye nguvu kiuchumi la G20 wamefanya mkutano wa dharura kwa njia ya video, wakiahidi kushirikiana katika kupambana na mripuko wa COVID-19 – pamoja na kutoa msaada mkubwa wa kifedha

   
Coronavirus - UN-Generalsekretär Guterres (Imago/L. Rampelotto)
Marekani imechukua jina baya la kuwa nchi yenye maambukizi mengi Zaidi ya virusi vya corona na kuripoti kuongezeka kwa rekodi ya ukosefu wa ajira, wakati viongozi wa ulimwengu wakiahidi dola trilioni 5 ili kuepusha kuporoka kwa uchumi wa dunia.

Zaidi ya watu 500,000 kote duniani sasa wameambukizwa virusi vipya vya corona, na kuilemea mifumo ya huduma ya afya hata katika mataifa tajiri na kusababisha msururu wa hatua za serikali kuwafungia raia majumbani mwao ambazo zimevuruga maisha ya mabilioni ya watu.

Nchini Marekani, Zaidi ya watu 82,000 wamethibitishwa kuambukizwa vurusi vya ugonjwa wa COVID-19, na kuipiku Italia, ambayo imeripoti vifo vingi Zaidi, na China, ambako virusi hivyo vilianzia mwezi Desemba mwaka jana katika jiji la Wuhan.

Huku hofu ikiendelea kuongezeka kuhusu mdororo wa kiuchumi ulimwenguni, viongozi kutoka kundi la nchi 20 zenye nguvu za kiuchumi la G20 walifanya mkutano wa dharura kwa njia ya video jana, wakiahidi kushirikiana katika kupambana na mripuko huo – pamoja na kutoa msaada mkubwa wa kifedha.

Viongozi hao wamesema katika taarifa kuwa "virusi hivyo havijali mipaka,” na kuahidi kutoa Zaidi ya Trilioni 5 katika uchumi wa ulimwengu, kama sehemu ya seraya kifedha, hatua za kiuchumi, na miradi ya dhamana ili kupambana na athari za kijamii, kiuchumi, na kifedha za janga hilo.

Aidha waliahidi msaada mkubwa kwa mataifa yanayoendelea, ambako virusi vya corona huenda vikasambaa baada ya kuvuruga China na kisha Ulaya.

Katika mkutano wa jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwaambia viongozi wa G20 kuwa "tupo katika vita na kirusi, na hatuonekani kushinda vita hivyo” licha ya hatua kubwa zinazochukuliwa na nchi mbalimbali kuifunga mipaka yake, kufunga biashara na kuamuru Zaidi ya robo ya watu duniani kubakia majumbani mwao. "Lazima tuwasaidie walio katika hatari kubwa. mamilioni kwa mamilioni ya watu ambao hawana uwezo wa kujilinda. hili ni suala la mshikamano wa kibinaadamu." Amesema Guterres.

Mkuerugenzi mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus aliwaambia viongozi wa G20 kuwa "tupo vitani na kirusi ambacho kinatishia kutuangusha – kama tutakiruhusu kufanya hivyo” ujumbe wetu kwa nchi zote ni wazi: Tii onyo hili sasa, uunge mkono mpango huu kisiasa na kiuchumi leo, na tutaweza kuokoa maisha na kupunguza kuenea kwa janga hili. historia itatuhukumu kwa namna tulivyozishughulikia jamii maskini kabisa katika wakati wao mgumu kabisa.

Saudi Arabien | G20-Finanzministertreffen in Riad (Imago iIages/photothek/F. Gärtner)
Saudi Arabia inashikilia urais wa G20 mwaka huu

Saudi Arabia, ambayo inashikilia urais wa G20 mwaka huu, iliufungua mkutano kwa ombi la dharura kutoka kwa Mfalme Salman kwa mataifa yenye nguvu Zaidi duniani kufadhili utafiti na utengengenezaji wa chanjo dhidi ya kirusi hicho.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki mkutano huo ni Boris Johnson wa Uingereza, Justin Trudeau wa Canada, Narendra Modi wa India, Vladmir Putin wa Urusi, Shinzo Abe wa Japan na Donald Trump wa Marekani. Mkutano huo pia uliwajumuisha Rais wa China Xi Jinping na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye alishiriki akiwa nyumbani kwake mjini Berlin ambako yuko katika karantini baada ya daktari aliyempa chanjo ya nimonia kupatikana na virusi vya corona. Aidha mkutano huo wa kilele pia uliwashirikisha viongozi wa Benki ya Dunia, shirika la Fedha la Kimataifa – IMF na Shirika la Kazi la Kimataifa - ILO