Wizara ya Elimu imejidhatiti kuongeza Mashirikiano na wadau wa Elimu


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe Simai Mohammed Said amesema Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa Elimu ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa kuzindua Mradi wa maji safi na salama  katika Skuli za Msingi na Sekondari,  uliodhaminiwa na Jumuiya ya (Time to help) ya jijini Dar es salaam katika ukumbi wa Wizara ya hiyo Mazizini mjini Unguja amesema upatikanaji wa maji safi na salama ni miongoni mwa miundombinu muhimu inayochangia  kuboresha Elimu nchini.

Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanya jitihada  kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma zote muhimu za jamii na kuendelea kuboresha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Nae Naibu Katibu Mkuu Utawala na Uendeshaji Mwalim Abdullah Mzee Abdullah amesema uchimbaji huo wa visima utafanyika katika baadhi ya Skuli za Msingi na Sekondari ambazo zina upungufu  wa maji safi na salama.

Amesema katika mradi huo Skuli 9 za Unguja na Skuli 5 za Pemba zitapata huduma hiyo ya visima vya maji  safi na salama ambapo Wizara ya Elimu itahakikisha Skuli hizo zinaweka sabuni za kunawia mikono kwa lengo la kuendelea kutunza mazingira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Time to help Bw Praph Ramadhan amesema Jumuiya yao itaendelea kutoa huduma za kijamii hasa sehemu ambazo baadhi ya huduma hazipatikani ili kuleta maendeleo katika jamii

Amesema Jumuiya yao imekua ikitoa huduma za maji, elimu na afya kwa watu wasiojiweza.

Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Feza Zanzibar Bw Ali Nungu  ametoa wito kwa Skuli zitakazobahatika kupata huduma hiyo kuitunza kwa hali na mali ili viendelee kuleta tija katika harakati za kila siku

Jumla ya Skuli 14 zitapata mradi huo zikiwemo  Mgambo, Muanda, Chunga, Dimani, Uzi ng'ambwa, Kandwi, Paje, Mtende na Sebleni kwa Unguja na kwa Pemba ni Wete, Pujini, Mizingani, Kijumbani na Mohd Juma Pindua ambapo Skuli sita za ziada zitafaidika baada ya kufanyiwa upembuzi yakinifu.