Madaktari tisa wafa kwa corona nchini Ufilipino


 Madaktari tisa wamekufa nchini Ufilipino kutoka na ugonjwa wa corona ambapo shirika la matibabu la juu la nchi hiyo limetangaza vifo hivyo.

Matangazo ya vifo vya madaktari hao tisa yameongeza hofu nchini humo huku ikionyesha kuwa hali ya maambukizi ya ugonjwa huo inaanza kukua ambapo sasa watu waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo ni watu 707 huku waliofariki kutokana na ugonjwa huo wakiwa ni watu 45.

Kisiwa kikuu cha Luzon, chenye takribani watu milioni 55, kipo katika kizuizi kwa wiki mbili sasa kwa lengo la kuzuia kuenea zaidi kwa virusi vya ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani.

Chama cha Madaktari cha Ufilipino wakati kikitangaza kifo cha daktari wa tisa kilisema kuwa chanzo cha madaktari hao kufa ni kukosekana kwa kinga ya kutosha kwa wahudumu wa afya nchini humo.

Hospitali tatu kubwa za Manila zilitangaza Jumatano kuwa walikuwa wamefikia uwezo wa mwisho na hawatakubali tena kupokea mgonjwa mpya wa virusi vya corona.

Mamia ya wafanyakazi wa matibabu nchini humo hawapo katika vituo vyao vya kazi kwa kuwa na wao wamejitenga kwa siku 14 baada ya kuwahudumia wagonjwa wa corona kwa muda mrefu.