ZEC Yataka Maoni Majimbo ya Zanzibar

TUME ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imewataka wadau wa uchaguzi nchini vikiwemo vyama vya siasa na wananchi kutoa maoni yao kuhusu idadi ya majimbo ya uchaguzi yaliyopo Zanzibar pamoja na mipaka ya shehia kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji mstaafu Hamid Mahmoud alisema mara ya mwisho Tume kufanya marekebisho ya majimbo ya uchaguzi Zanzibar ilikuwa mwaka 2015 ambapo majimbo yaliongezwa kutoka 50 hadi kufika 56.

Alisema tangu mwaka 2015 ni kipindi kirefu na kuwa yapo mabadiliko makubwa katika majimbo ya uchaguzi ikiwemo mipaka hadi idadi ya wakazi wake wameongezeka. Kwa mfano alisema yapo malalamiko zipo wadi ambazo shehia zake zinahudumiwa na majimbo mawili tofauti kinyume na utaratibu,ambapo kwa kawaida jimbo linaundwa na wadi mbili hadi tatu.

Aidha alisema yapo majimbo idadi ya wapiga kura imeongezeka kutokana na uhamiaji na watu wenye sifa za kupiga kura kutimiza umri kamili na kuwa marekebisho yanahitajika.

Aidha Jaji mstaafu Mahmoud alisema maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 yanaendelea vizuri na kuzitaja hatua zilizofikiwa ikiwemo kukamilisha uchapishaji wa nyaraka,uagiziaji na ununuzi wa vifaa mbali mbali vya uchaguzi mkuu.

Hatua nyingine zilizochukuliwa na kufikia hatua nzuri kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba ni kuhakiki taarifa za daftari la kudumu la wapiga kura kazi ambayo ilianza Januari 18, 2020 katika wilaya ya Micheweni Pemba na kukamilika Machi 3, mwaka huu katika wilaya ya mjini magharibi Unguja.

Alisema uhakiki huo umefanikiwa na kuwaingiza watu wenye sifa katika daftari hilo tayari kwa matayarisho ya uchaguzi mkuu pamoja na wapiga kura wapya waliofikisha umri wa miaka 18.

Jaji Mahmoud alisema katika takwimu za awali za watu walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura walikuwa 413,444 ambapo 199,327 ni wanaume na 214,117 walikuwa wanawake.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia