Kashfa ya mauaji ya mke yamng'oa madarakani waziri mkuu Lesotho



Thomas Thabane ametangaza kuwa atajiuzulu kama waziri mkuu wa Lesotho kufuatia miezi kadhaa ya shinikizo baada ya kutajwa kama mshukiwa katika mauaji ya aliyekuwa mkewe.

Hakusema ataachia madaraka lini lakini chama chake kimesema kuwa waziri mkuu mpya ataapishwa Jumatano.

Mke wa Thabane wa sasa (mke mdogo), ambaye alikuwa akiishi naye wakati aliyekuwa mkewe anauawa, alishtakiwa mwezi Februari kwa kuhusishwa na mauaji hayo.

Thabane mwenye miaka 80, na mkewe mdogo wamekanusha kuhusiaka na mauaji ya mke mkubwa.

"Nimeamua kuja na kuwaarifu kuwa nitajiuzulu kama waziri mkuu wa Lesotho," shirika la habari la AFP limesema aliwambia wafuasi wake katika mji wake wa nyumbani wa Abia viungani mwa mji mkuu wa Maseru.

Lesotho imeghubikwa na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa mwaka huu - na waziri huyo mkuu alipoteza wingi wa viti bungeni wiki jana pale muungano unaomuunga mkono uliposambaratika na serikali mpya inatarajiwa kushika usukani Ijumaa hii.

Wanaume waliokuwa wamejihami kwa silaha walimpiga risasi na kumuua Lipolelo Thabane Juni 14, 2017 - siku mbili kabla ya Bwana Thabane kuapishwa kama waziri mkuu.


Akiwa njiani wakati anarejea nyumbani, alivamiwa, na kupigwa risasi mara kadhaa na kuaga dunia kando kando ya barabara ya vumbi akiwa na umri wa miaka 58.

Wakati huo, Lipolelo alikuwa anapitia kipindi kigumu baada ya kutalakiana na Bwana Thabane na alikuwa akiishi peke yake tangu 2012.

Thabane alikuwa amesonga mbele na maisha yake na mwanamke mpya, Maesaiah Thabane, kati ya 2012 na 2017.


Bwana Thabane, 80, ni mmoja kati ya viongozi wakongwe Afrika na kwa kipindi kirefu maishani mwake amekuwa mwanasiasa.

Anafahamu vyema kuhusu suala la upinzani wa kisiasa, Bwana Thabane kuna kipindi aliwahi kutorokea Afrika Kusini kwa madai ya kupanga njama ya mapinduzi na jeshi na alilazimika kusindikizwa hadi nchini Lesotho na maafisa wa polisi.

Februari, wakili wake alikuwa mahakamani alidai kwamba mteja wake, nafasi anayoshikilia uongozini kama waziri mkuu inampa kinga dhidi ya kushtakiwa.

Kesi hiyo ilihamishwa hadi mahakama kuu lakini mahakama hiyo bado haijaisikiliza.

Haijafahamika kwanini kesi hiyo imechukua muda mrefu kutajwa katika mahakama hiyo.

Bwana Thabane anasisitiza kuwa shutuma dhidi yake zinachochewa kisiasa.

Huenda ikawa pengine ni kwasababu alikuwa anajitahidi kujadiliana na chama chake kufikia makubaliano kuwa uchunguzi dhidi yake ungefutuliwa mbali iwapo angejiuzulu.
Ikiwa ilikuwa hivyo, hadi kufikia sasa njia hiyo bado haijafanikiwa.

Msemaji wa chama cha Bwana Thabane, cha All Basotho Convention (ABC), aliarifu kituo cha BBC, Pumza Fihlani kwamba hakitaunga mkono hatua yoyote ya kupata kinga ya kumlinda ili asishtakiwe.

Amekuwa akipinga shinikizo la juu kutoka kwa chama chake la kumtaka ajiuzulu tangu mwanzo.

Karibia na wakati waziri huyo anafika mahakamani, alitangaza kwamba hatajiuzulu hadi Julai.

Alitaja umri mkubwa kama moja ya sababu ya kujiuzulu kwake lakini hakuzungumza lolote kuhusu kesi ya mauaji inayomkabili.

Aprili, wapatanishi kutoka Afrika Kusini walijadiliana kuhusu makubaliano yaliyomuahidi kuachia madaraka kwa heshima.


Lakini siku chache baadae, alinukuliwa kusema kwamba hatashinikizwa na mtu kuondoka madarakani hadi pale atakapokuwa tayari kuondoka na kwamba hakuna aliyekuwa na haki ya kuweka muda wa yeye kuachia madaraka.

Waziri wa fedha wa sasa Moeketsi Majoro, anaonekana kuwa tayari kushika usukani wa waziri mkuu. Amechaguliwa kuwa kiongozi wa muungano mpya unaotawala na chama cha ABC na washirika wake, na kile cha DC (Democratic Congress).

Mfalme wa Lesotho - utawala mdogo unaozungukwa na Afrika Kusini - anafahamishwa rasmi na inatarajiwa kwamba Bwana Majoro ataapishwa katika makazi ya mfalme mji mkuu wa, Maseru, Jumatano.


Kisha Bunge litaanza tena vikao vyake Ijumaa, wakati ambapo serikali mpya inatarajiwa kuapishwa.