China yatoa radiamali kuhusu kifo cha balozi wake huko Israel


Gazeti moja la China limeandika kwamba, kifo cha balozi wa nchi hiyo katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kilitokea baada ya yeye kukosoa siasa chafu za kupenda kujitanua za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo.

Gazeti la South China Morning Post limeinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya China ikisema kuwa Du Wei (57) balozi wa nchi hiyo huko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni amefariki dunia katika hali isiyo ya kawaida. Limeongeza kwamba Beijing itatuma wataalamu wake kuchunguza sababu za kifo cha mwanadiplomasia huyo na pia kuusafirisha mwili wake. Hii ni katika hali ambayo polisi wa utawala bandia wa Israel walikuwa wamejizuia kutangaza sababu za kifo cha balozi huyo wa China.


Kanali ya televisheni ya 12 ya utawala wa Kizayuni imetangaza kwamba Du Wei alifariki dunia katika hali ya kawaida akiwa usingizini nyumbani kwake. Hivi karibuni, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliikosoa vikali serikali ya China akiituhumu kuwa inahusika na kuenea kwa virusi vya Corona duniani, huku kwa upande wake serikali ya Beijing ikiituhumu Marekani kuwa chanzo kikuu cha virusi hivyo nchini China na katika mataifa mengine ya dunia.

 Siku chache zilizopita gazeti la Jerusalem Post la Israel lilichapisha taarifa iliyotolewa na Bwana Du Wei akimkosoa vikali Mike Pompeo na siasa za Marekani za kupenda kujitanua.