Virusi vya corona: WHO iliwacha mlipuko 'ukashindwa kudhibitika', yasema Marekani


Marekani imelishutumu shirika la Afya duniani kwa kuruhusu Covid -19 kushindwa kudhibitika kwa gharama ya maisha mengi.

''Shirika hili lilifeli kupata habari ambayo ulimwengu ulihitaji'', alisema waziri wa Afya wa Marekani Alex Alazar.

Bwana Alazar alitoa matamshi hayo katika hotuba kwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Katibu mkuu wa Shirika la Afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus awali alikubali kwa uchunguzi ambao utaweka wazi jinsi shirika hilo lilivyoangazia mlipuko huo.

Dkt. Tedros amesema kwamba uchunguzi huru ambao utatazama mafunzo na kutoa mapendekezo utafanyika mapema.

Mkutano huo wa siku mbili - unaofanyika kila mwaka na unaohusisha nchini 194 wanachama wa WHO huangazia kazi ya shirika hilo na unajiri wakati ambapo kuna vita vya maneno kati ya china na Marekani kuhusu virusi hivyo.

Rais wa Marekani Donald Trump , ambaye anakabiliwa na uchaguzi mkuu mwaka huu ambaye amekosolewa jinsi anavyotatua ugonjwa huo nchini Marekani , amelaumu China kwa kujaribu kuziba mlipuko huo na kuilaumu WHO kwa kushindwa kuiwajibisha China.

Rais wa China Xi Jingpin , ambaye ametetea vitendo vya China wakati wa mlip[uko huo , alisema katika mkutano huo kwamba taifa lake lilikabiliana na ugonjwa huo kwa uwazi na kusisitiza kwamba uchunguzi wowote ufanyike baada ya mlipuko huo kudhibitiwa.

Aliongezea China itatoa $2bn katika kipindi cha miaka miwili ili kusaidia mataifa duniani na kutoa ombi la kugawanya chanjo itakapokuwa tayari.

Wakati huohuo rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema kwamba WHO inafaa kupewa uwezo wa kisheria kuhakikisha kuwa matafa yanaripoti milipuko na kupeana data.

Mlipuko mwengine hatari wa magonjwa ya maambukizi unaweza kutokea wakati wowote na ni muhimu tuweze kukabiiana nao haraka iwezekanavyo, alisema.

Zaidi ya watu milioni 4.5 wameambukizwa na zaidi ya 300,000 wamefariki tangu virusi hivyo kutokea chini China mwezi Disemba.