KENYA: Familia 600 zaachwa bila makao baada ya nyumba kusombwa na mafuriko Lamu




ZAIDI ya familia 600 zimeachwa bila makao baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko katika vijiji vya wadi za Witu, Mkunumbi na Hongwe, Kaunti ya Lamu.

Katika wadi ya Witu, nyumba 87 za kijiji cha Moa, 70 kwenye kijiji cha Chalaluma na 56 katika kijiji cha Dide Waride zilikuwa zimezingirwa na maji yanayosababishwa na kuvunjika kwa kingo za Mto Tana na ule mdogo wa Nyongoro kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika maeneo hayo.

Vijiji vingine ambavyo wakazi wameathiriwa na mafuriko ni vile vya wadi za Mkunumbi na Hongwe, ikiwemo Marafa, Jericho, Jipendeni, Salama, Lumshi, Zebra, Juhudi, Sinambio, Mavuno, Amkeni na sehemu zingine.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Msalaba Mwekundu, tawi la Lamu, jumla ya familia 445 zimeathiriwa na mafuriko katika vijiji hivyo.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Afisa Mshirikishi wa Msalaba Mwekundu, Kaunti ya Lamu, Bi Kauthar Alwy, amesema Jumamme kwamba ofisi yake tayari imetuma timu maalum kwenye maeneo yote yanayoshuhudia mafuriko ili kutathmini hali na kuandaa ripoti itakayobaini idadi kamili ya waathiriwa wa mafuriko eneo hilo kabla ya kupeleka misaada kwa wanaohitaji.

“Kuna vijiji zaidi ya 10 ambavyo vimekumbwa na mafuriko na tayari tumetuma timu ya maafisa wa Msalaba Mwekundu kuingia vijijini humo ili kutathmini hali na kuandaa ripoti,” amesema Bi Alwy.
Amesema kufikia wakati tunachapisha taarifa hii, familia zipatazo 445 kwenye vijiji vya wadi za Mkunumbi na Hongwe pekee ndizo zilikuwa zimethibitishwa kuathiriwa na mafuriko hayo.

Akaongeza kwamba idadi huenda ikaongezeka kwani wamepokea habari kwamba vijiji vya Chalaluma, Moa na Dide Waride, wadi ya Witu pia vimeathiriwa na mafuriko hayo.

Baadhi ya wakazi katika vijiji husika wameiomba serikali na wahisani kuwasaidia kwani wanateseka baada ya nyumba zao kubomolewa na mafuriko hayo.

Mwenyekiti wa Nyumba Kumi kijijini Chalaluma, Bonea Abadima, ameeleza wasiwasi wake kwamba huenda wakaambukizwa maradhi yanayosababishwa na maji machafu yaliyozingira nyumba zao.

“Vyoo vimebomolewa na mafuriko. Wakazi wa hapa wanatumia maji hayo hayo kwa matumizi ya nyumbani. Kuna hatari ya mkurupuko wa kipindupindu wakati wowote hapa,” amesema Bw Abadima.

Naye Bi Zeinab Kulisa ameiomba serikali ya kaunti na Shirika la Msalaba Mwekundu kuwapelekea chakula na vyandarua ili kujikinga dhidi ya mbu.

Amesema wamelazimika kutafuta makao kwenye nyanda za juu lakini hawana mahema ya kutundika ili kujikinga dhidi ya mvua.

“Tunateseka hapa tangu mafuriko yasombe nyumba zetu. Hatuna pa kulala. Mbu wamesheheni ilhali hatuna vyandarua vya kujikinga. Isitoshe, chakula pia ni shida. Tunaomba serikali na wahisani, ikiwemo Shirika la Msalaba Mwekundu kutusaidia. Tuko na hofu ya watoto wetu kupata malaria hapa,” amesema Bi Kulisa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia amesema ofisi yake pamoja na wadau wengine tayari wameanza harakati za kusambaza chakula cha msaada kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.

Bw Macharia aidha amewataka wakazi wanaoishi maeneo ya nyanda za chini kuhamia nyanda za juu ili kuepuka hasara zaidi inayoletwa na mafuriko.

“Lazima wananchi wachukue tahadhari ya mapema kwa kuhamia maeneo salama wakati huu wa mvua kubwa inayoandamana na mafuriko,” amesema Bw Macharia.