Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Ijumaa amejibu matamshi ya kuchekesha ya Brian Hook, mwakilishi maalumu wa serikali ya Marekani katika masuala ya Iran na kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, taifa kubwa la Iran limesambaratisha mashinikizo ya kiwango cha juu ya Washington kwa muqawama wa kiwango cha juu, imani isiyotetereka na kwa kutegemea uwezo wake wa ndani.
Sayyid Abbas Mousavi ameongeza kuwa, Marekani imma ikubali kuwa imeshindwa na hivyo ifuate njia ya kuliheshimu taifa la Iran au ikubali kuendelea kudhalilika, kuchukiza na kutengwa kimataifa.
Katika mahojiano aliyofanyiwa juzi na mtandao wa Kizayuni wa Jewish News Syndicate, Brian Hook alitoa matamshi ya kuchekesha alipodai kuwa, kutokana na mashinikizo ya kiwango cha juu ya Washington, sasa viongozi wa Iran wanapaswa waamue imma kufanya mazungumzo na Marekani au nchi yao isambaratike kiuchumi.
Baada ya Marekani kujitoa kijeuri kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, iliiwekea vikwazo Iran ambavyo wakuu wa Washington wanajigamba kuwa ni vya kiwango cha juu sana kuwahi kuwekewa taifa lolote lile duniani.
Siku ya Jumanne ya tarehe 8 Mei 2018, Donald Trump aliitoa Marekani kwenye mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA licha ya makubaliano hayo kuwa na baraka zote za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na aliirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya makubaliano hayo.
Hatua hiyo ya kibeberu na kijeuri ya Marekani inaendelea kulaaniwa hadi leo hii kote ulimwenguni.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni moja ya nguzo kuu za kambi ya muqawama, ina mchango mkuu katika kubatilisha njama za kundi la Marekani, Wazayuni na Wasaudi.

