Wabunge wa Iran wachagua spika mwenye msimamo mkali


Wabunge wa Iran leo wamemchagua kamanda wa zamani wa jeshi la anga la jeshi la walinzi wa mapinduzi Mohammad Qalibaf kuwa spika wa bunge jipya linalodhibitiwa na idadi kubwa ya wanasiasa wa msimamo mkali.

Televisheni ya taifa nchini Iran imeripoti kuwa wabunge 230 kati ya 264 wamempigia kura Qalibaf ambaye pia ni meya wa zamani wa mji mkuu Tehran kuliongoza bunge hilo kwa muda wa mwaka mmoja Rikodi yake ya kuwa mpiganaji katika vita vya miaka ya 1980 kati ya Iran na Iraq pamoja na wakati akiwa mkuu wa polisi ya taifa imemjengea wasifu wa kuaminika mbele ya kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.

Ingawa bunge la Iran lenye viti 290 halina ushawishi mkubwa katika sera ya kigeni kuhusu suala la mradi wa nyuklia, kuchaguliwa kwa Qalibaf kunaweza kuwasaidia wanasiasa wa msimamo mkali katika uchaguzi wa rais wa mwaka unaokuja na kuimarisha sera ya mambo ya kigeni ya Iran.