Halmashauri ya Masasi yapata hati safi ukaguzi hesabu

Na Hamisi Nasiri, Masasi


  HALMASHAURI ya Mji Masasi Mkoani Mtwara imefanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu zake kutokana na utendaji wake wa ukusanyaji mapato kwenye vyanzo vyake vya ndani katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, 2019
  Kulingana na ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali(CAG) hati safi hutolewa pale anaporidhirika kuwa taarifa za fedha ziliandaliwa kwa kuzingatia viwango vya uandaaji wa hesabu vinavyokubalika kwa kiasi kikubwa,hii ina maana kuwa taarifa za fedha hazina makosa makubwa.

  Hayo yamebainishwa jana wilayani Masasi na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Gimbana Ntavyo wakati wa baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo lililofanyika kujadili hoja za taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19
   Alisema kuwa,halmashauri imepata kutokana na watendaji wake na Madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano katika suala zima la kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa kiwango kinachotakiwa.
   Ntavyo alisema katika ukaguzi huo wa hesabu za serikali(CAG) kuanzia Julai mosi mwaka 2018 hadi mwezi Juni 2019 ,halmashauri ya mji Masasi ilikuwa na jumla ya hoja 20 ambapo kati ya hoja hizo, hoja tisa zilipatiwa majibu na kufungwa.

   Alisema hoja moja ilihamishiwa Mamlaka ya maji vijijini (Ruwasa) huku hoja 10 bado zinaendelea kufanyiwa kazi hivyo kwa msingi huo halmashauri inakidhi vigezo vya kupatiwa hati safi ya hesabu za serikali.

 “Upatikanaji wa hati hii ya safi unatokana na ushirikiano wetu kati ya watendaji pamoja na Madiwani hivyo naomba ushirikiano huu uendelee kuwepo daima,”alisema Ntavyo
  Akifunga kikao hicho,Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Gelasius Byakanwa aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi ya hesabu za serikali.

   Aidha,Byakanwa ameagiza menejimenti ya halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya badala ya kutegemea vyanzo vile vile kila siku.
 “Menejimenti hakikisheni mnakuwa na kasi kubwa ya katika kukusanya mapato kwani ndio yatakayowafanya muweze kuwa na fedha za kutosha katika kuendesha halmashauri yenu bila ya mapato mtakwama,”alisema Byakanwa

  Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Sospeter Nachunga Madiwani wa halmashauri hiyo wapo mbioni kumaliza muda wao lakini wataondoka huku halmashauri hiyo ikiwa katika mazingira mazuri ya ukusanyaji wa mapato.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items