Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema hujuma ya kigaidi ya ISIS au Daesh dhidi ya Bunge la Iran ilikuwa nembo ya ndoto chafu za maadui wa taifa la Iran.
Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo leo katika kikao cha bunge alipozungumza kwa mnasaba wa kumbukumbu ya hujuma ya magaidi wa ISIS dhidi ya Bunge la Iran na Haram Takatifu ya Imam Khomeini (MA) mjini Tehran.
Qalibaf amesema mashirika ya kijasusu ya Marekani, Israel na baadhi ya nchi za eneo yalihusika na hujuma hiyo na walikuwa na mpango wa kuwaua watu katika mitaa ya Tehran.
Katika hujuma hiyo ambapo magaidi wakufurishaji wa kundi la ISIS waliolenga Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na Haram Takatifu ya Imam Khomeini (MA) mnamo 7 Juni 2017 mjini Tehran, watu 17 waliuawa shahidi na wengine kadhaa walijeruhiwa. Wote waliotekeleza hujuma hiyo waliangamizwa.

