Pompeo azungumza kwa simu na kiongozi wa Taliban


Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, amempigia simu na kuzungumza na mkuu wa timu ya wapatanishi wa kundi la Taliban, kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo, katika wakati ambapo Washington imekumbwa na mtafaruku kufuatia kuibuka kwa madai kwamba Urusi ilikuwa ikiwalipa Wataliban kuwauwa wanajeshi wa Marekani na NATO nchini Afghanistan.

Taliban inakanusha madai hayo. Haijulikani endapo Pompeo na Mullah Abdul Ghani Baradar walizungumzia suala hilo kwenye mkutano wao kwa njia ya vidio uliofanyika jana, lakini Waziri huyo wa masuala ya kigeni wa Marekani alilitaka kundi hilo kupunguza mashambulizi yake nchini Afghanistan.

Viongozi hao wawili walijadiliana njia za kuendelea na mkataba wa amani uliosainiwa kati ya Marekani na Taliban mwezi Februari mwaka huu, kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo, Suhail Shaheen.