Siku moja baada ya Serikali ya Rwanda kutuma risala ya pongezi kwa rais mteule wa Burundi Meja Jenerali Everiste Ndayishimiye mjadala umeibuka ikiwa nchi hiyo ina nia ya kukomesha mzozo kati yake na Burundi.
Hii ni baada ya Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Rwanda kutumia fursa hiyo kusema kwamba nchi hiyo iko tayari kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo.
Rwanda na Burundi ni nchi zenye kabila,utamaduni na lugha moja lakini uhusiano wao ulikuwa mbaya tangu mwaka 2015 kufwatia uchaguzi wenye utata wa rais Pierre Nkurunziza anayeondoka madarakani.
Tangu wakati huo nchi hizo mbili zimekuwa zikishutumiana kuunga mkono makundi ya waasi kutoka kila upande.Risala ya pongezi kwa rais mteule wa Burundi jenerali Evariste Ndayishimiye imetumwa na Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Rwanda ambayo imepongeza serikali ya Burundi kwa uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita.
Ni risala iliyozua hisia mbali mbali kwenye mitandao ya kijamii,raia wa Burundi na raia wa Rwanda wakichangia maoni. Badhi yao wamepongeza hatua hiyo.
Kuna waliohoji kwa nini siyo rais wa Rwanda Paul Kagame aliyempongeza rais mteule wa Burundi kama ilivyotokea kwa marais wengine wa mataifa ya Kenya,Tanzania na Uganda na badala yake risala hiyo kuandikwa na wizara ya mambo ya nchi za nje.
