Ujerumani yataka kuwataja wakiukaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa nchini Libya


Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, ameapa kwamba atazitaja kwa majina nchi zinazovunja vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya, ikiwa ni njia ya kuzishinikiza kuacha kuchochea machafuko na mauaji.

Kwenye mazungumzo yake na shirika la habari la Ujerumani, dpa, Maas amesema kwamba mtu hawezi kuepuka kuwataja kwa majina wakiukaji hao, na kwamba dhamira ya kufanya hivyo inazidi kukuwa ndani ya Umoja wa Ulaya.

Umoja huo umeanzisha operesheni ya majini kufuatilia marufuku ya silaha iliyowekwa na Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya miaka tisa sasa.

Ingawa ufuatuliaji kwa njia ya satalaiti umebaini silaha hizo zikiingizwa nchini Libya, hadi sasa imeshindikana kuzizuwia. Hadi sasa, taarifa kuhusu ukiukwaji wa vikwazo hivyo zinapelekwa tu Umoja wa Mataifa, ambapo hivi karibuni Katibu Mkuu wake, Antonio Guterres, alizitaja Uturuki, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi kuwa miongoni mwa wakiukaji wakubwa.