Vyama vya siasa 12 vyamtaka msajili wa vyama kumchukulia hatua Maalim Seif

VYAMA vya Siasa 12 vimeitaka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kumchukulia hatua kali za kisheria Mwenyekiti wa chama cha ACT wAZALENDO,Maalim Seif Sharif Hamadi kwa kutoa kauli za kichochezi ambazo anaenda kinyume na kanuni na sheria za vyama vya siasa nchini.

Pia wamesema kiongozi huo ametoa kauli ambazo zinalengo la kuhatarisha amani na kuchochea uvunjifu wa amani ulipo visiwani humo.

Kauli hiyo imetolewa kwa waandishi wa habari  na Katibu Mkuu wa Chama cha Democrasia Makini, Ameir Hassan Ameir kwa niaba ya vyama 12 vya upinzani ambavyo ni Demokrasia Makini, DP,SAU,TLP,UPDP,CCK,NLD,NCCR,ADA TADEA,AFP,ADC,UDP.


TAMKO LA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA ZANZIBAR KWA WANAHABARI  KUHUSIANA NA MAMBO MBALIMBALI YANAYOENDELEA NCHINI LEO TAREHE
25 JUNI, 2020
KATIKA UKUMBI WA BARAZA LA WAWAKILISHI LA  ZAMANI - ZANZIBAR

Ndugu Wanahabari  Assalamu alaikum,

Awali ya yote, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa niaba ya viongozi wezangu wa vyama vya siasa,  kwa kutujaalia kukutana hapa asubuhi hii, ili kuuhabarisha umma juu ya mambo mbali mbali yanayoendelea kutokea hapa nchini kwetu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Pia, niwashukuru nyinyi wanahabari kuja kuungana nasi, na imani yetu, mkitoka hapa mtafanya kazi yenu kwa uadilifu na taarifa hii wananchi waifahamu kwa mstakbali mzuri wa nchi yetu.

Ndugu wanabari

Kama mnavyo fahamu, nchi yetu imekabiliwa na uchaguzi mkuu  mwezi wa October 2020. Na ukweli, tayari harakati zimeanza kwa vyama vya siasa na wadau wa siasa mbali mbali, kwa kuanza harakati zakisiasa. Lakini pia, tukumbuke nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu tulizojiwekea na hakuna mtu yeyote alie juu ya sheria.

Ndugu wanabari

Tayari kumeibuka tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, kwa  kujinaasibu na kuanza kuwahamasisha wafuasi wao kuanza kujipanga kwa chochote kitakacho tokea na kuwa tayari kulinda ushindi kwa nguvu zote na kwa hali yoyote


.

MIKAKATI  YA  KULETA  FUJO  HAIKUBALIKI  ZANZIBAR

Tukiwa kama wakaazi na viongozi wa visiwa hivi vya Unguja na Pemba hatukubaliani na hatuwezi kuunga mkono kauli zozote zinazoashiria kuhamasisha uvunjifu wa amani kwa kisingizio chochote kile.

Ndugu wanabari

Kauli kama “Enough is Enough” “Lazima tujipange kwa lolote”       “ kama noma na iwe noma”  kauli kama hizi zilizotolewa na Maalim Seif kiongozi wa ACT Wazalendo ni kauli za kuleta Uchochezi kwa lengo la kuanza kuleta fujo na vurugu na kupelekea uvunjifu wa  amani kwa Wanzanzibari na Watanzania, na hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika uchaguzi mkuu na kuanza kuwatia hofu wananchi pamoja na kuhatarisha amani iliyoko hapa nchini kwetu.

Ndugu wanabari

 Maalim Seif pamoja ya kuwa ni mwanasiasa mkongwe, anafahamu kutokana na umri wake, uchaguzi wa mwaka huu unaweza kuwa wa mwisho kugombea kutokana na umri wake, na hasa  kama akikosa nafasi anayotaka kugombania. Maana yake ni kwamba  ile hamu yake ya miaka nenda miaka rudi kuwa Rais wa Zanzibar itakuwa imekufa kifo cha mende. Na ndio maana, ameanza kutafuta Visingizio na kupanga kuleta fujo, ili kuwaonesha maswahiba wake wanaomfadhili.   

Lakini pia, tumeona kutokana na hali halisi iliyoko Zanzibar hasa kwa uungwaji mkono mkubwa wa vyama vyetu vya upinzani, ambavyo vinakataa fujo na tumekuwa mstari wa mbele  kuhamasisha  amani na utulivu uliopo, hali hii imemtisha Maalim Seif, kwa kuona anaweza kushindwa tena kwa aibu mara hii katika Uchaguzi.  Hivyo basi, tabia ya kuleta vurugu, kutoa maneno ya kashfa  na kususia uchaguzi ndio imekuwa tabia yake na viongozi wenziwe ambao hawaitakii mema nchi yetu.

Ndugu wanabari

Sisi viongozi wa vyama vya siasa, tunamshauri Maalim Seif Sharif Hamadi pamoja na wenzake kwanza wasikimbie uchaguzi, na wala wasiandae vurugu kwani Wanzanzibar na Watanzania kwa ujumla tunahitaji Amani yakudumu na kudumisha utulivu wakati huu kuliko wakati mwengine wowote.

Ndugu wanabari

Tunaomba  kutowa wito kwa wanasiasa wenzatu, tuache tabia ya kutafuta uhasama na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kutoa shutuma ambazo hazina ukweli wowote juu yao. Pia kupotosha umma kwa kisingizio cha kuhusika na kujishughulisha na mambo ya siasa jambo ambalo sio la kweli, kwani kwa mujibu wa sheria miongoni mwa kazi zao ni pamoja na kulinda usalama wa raia na mali zake. Hivyo, kitendo cha kuwapaka matope hakina tija kwa Taifa letu.

Ndugu wanabari

 Pia, tunachukuwa fursa hii kwa kuwatahadharisha  wananchi juu ya  kauli ya Maalim Seif ya kuwataka wafuasi wake kuwa tayari kwa lolote kwa kuwaambia wafuasi wake  “ WAKIFANYA SUU NA NYINYI FANYENI SWAA”  na kauli ya “HAKUNA TENA KURUDI NYUMA” Tujiulize, kauli kama hizi zinamsingi gani kwa amani ya nchi yetu?

Sisi viongozi wa vyama vya Siasa, tunaamini kupitia  kauli kama hizi na nyengine anazozitoa, ni wazi amejiandaa kujihami na kuhamasisha wafuasi wake kujiandaa na fujo na kuufanya uchaguzi Mkuu wa mwaka huu usifanyike kwa amani na utulivu au baada ya matokeo kutokubaliana na matokeo hayo.
Pia, tunasikitishwa na maombi aliyoyatoa kwenye kikao chake cha ACT Dar es Salaam, kwa kuwahamasisha vijana kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar kuwasaidia, swali tunalojiuliza waje kufanya nini?         Kupitia taarifa hii tunaviomba vyombo vya Ulinzi na Usalama kutodharau kauli kama hizi kwani waswahili wanasema “ Usipoziba ufa utajenga ukuta”.

Ndugu wanabari

Kupitia kauli zilizosambaa katika mitandao ya kijamii za kiuchochezi zinazotolewa na Maalim Seif kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo tunaviomba vyombo vya Ulinzi na usalama kufuatilia kwa makini kauli hizi na kuzichukulia hatua kabla na baada ya Uchaguzi.
Pia, tunaiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini,  kuchukuwa hatua za haraka , kwani tabia hii imezoeleka ilhali kanuni na  sheria za vyama vya siasa ziko wazi kwa kila anaenda kinyume na Sheria hizo.
Kifungu cha 9 kifungu kidogo cha 2(f) kinakataza mwanachama wa chama cha siasa kutumia lugha ya matusi, dhihaka, kuudhi na uchochezi katika shughuli za kisiasa  inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Hivyo, kutumia lugha za uchochezi ni kukiuka sheria ya vyama vya siasa. Msajili anaaswa kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya chama kinachokiuka sheria ya vyama vya siasa hasa wakati huu nyeti wa maandalizi ya chaguzi. Kwa mujibu wa sheria hii chama hicho kifutwe au usajili wake usimamishwe ili kisiweze kushiriki uchaguzi kikaleta vurugu. Pia, mwanachama wa chama husika aliefanya au waliofanya vitendo hivyo, waadhibiwe wao wenyewe kama sheria ya vyama vya siasa inavyoelekeza. Na ikiwezekana apewe au wapewe adhabu ya kusimamishwa wasifanye shughuli za kisiasa ikiwemo kushiriki uchaguzi.

Ndugu wanabari
Sisi viongozi wa vyama vya siasa ni wajibu wetu kutii na kufuata sheria ya vyama vya siasa.  Hivyo,  Mh Msajili tunakuomba uchukuwe  hatua kwa kila anaekwenda kinyume,  kudharau au  kukejeli  sheria.

Mwisho, Tunawaomba wananchi kuwa macho, kwa  kutokubali kuhamasishwa katika kuleta vurugu, kupandikizwa chuki, na kishirikishwa katika mambo yanayo hamasisha uvunjifu wa amani  katika visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla. Historia inaonesha, kila tukikaribia  katika uchaguzi wasiopenda amani na utulivu katika Taifa letu,  huanza harakati zakuvuruga amani iliyopo  hasa wakati kama huu kwani tumeshuhudiya miundombinu mbali mbali ikiharibiwa kutokana nakufuata kauli kama hizi .
Sisi viongozi wa vyama vya siasa, tunazishauri Serikali zote mbili ya Zanzibar na Tanzania  kuchukuwa hatua za haraka kwa kuwadhibiti wale wote wasiokuwa na nia njema  na kuhamasisha wafuasi wake kujiandaa kufanya vurugu  pamoja na  kila anaejaribu kuhatarisha amani ya nchi yetu. Kwani Wazanzibar  na Watanzania wote wanahitaji amani.

Tamko hili limesomwa kwenu na mimi Katibu Mkuu wachama cha Demokrasia MAKINI , Ameir Hassan Ameir, kwa  niaba ya Viongozi wa vyama vya siasa.

1. DEMOKRASIA MAKINI
2. DP
3. SAU
4. TLP
5. UPDP
6. CCK
7. NLD
8. NCCR
9. ADA TADEA
10. AFP
11. ADC
12. UDP 
                     NIWASHUKURU   KWA   KUNISIKILIZA.