Afrika Kusini yarudisha marufuku ya uuzaji vileo kukabili corona


Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amerudisha tena amri ya kutotoka nje usiku nchini mwake, pamoja na marufuku dhidi ya uuzaji wa vileo, mnamo wakati maambukizi ya virusi vya corona yakiongezeka na mfumo wa afya ukitishiwa kulemewa.

 Katika siku za hivi karibuni, Afrika Kusini imekuwa ikirekodi visa vipya 12,000 kila siku, hiyo ikiwa ni sawa na maambukizi 500 kila saa. Hali hiyo imesababisha shinikizo kubwa kwa mfumo wa afya nchini humo.

 Afrika Kusini ndilo taifa ambalo limeathiriwa zaidi barani Afrika, likiwa limerekodi jumla ya visa 276,242, pamoja na vifo 4,079. Rais Ramaphosa ameonya kwamba janga la corona alilolitaja kuwa 'dhoruba ambalo limeikumba nchi yake' ni janga hatari lenye uharibifu mkubwa kuwahi kulikumba taifa hilo.