Kamati ya CCM mkoa wa Ruvuma imekagua miradi mbali mbali ukiwemo wa chuo cha veta nyasa



KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma imekagua mradi wa ujenzi wa  chuo cha ufundi stadi VETA Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ambao unagharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa,Jimson Mhagama  amesema mradi unahusisha majengo 16 na kwamba fedha za mradi zimepokelewa kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza zimepokelewa zaidi ya bilioni moja.



Amesema mradi huo unatekelezwa  na mafundi mawili wakiwemo SUMA JKT ambaye anajenga majengo 14 na Simon Chiwanga ambaye anajenga vyumba viwili vya madarasa na kwamba mradi umetoa jumla ya ajira 123.

Mhagama amesema mradi huo unatekelezwa kwa kutumia mtindo wa force account ambapo wananchi kutoka Kata ya Kilosa ambako mradi unatekelezwa wanashiriki  na kwamba mradi ulianza Februari 21,2020 na unaarajiwa kukamilika Julai 31 mwaka huu.

Hata hivyo amesema mradi umefikia katika hatua tofauti za utekelezaji ambapo majengo saba yamefikia zaidi ya asilimia 80 ambayo ni nyumba ya Mkuu wa Chuo,kibanda cha mlinzi,vyumba viwili vya madarasa ,karakana na vyoo.


“Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa kushirikiana na wananchi tunaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kupitia mradi huu ambao utawanufaisha vijana wa Nyasa’’,alisisitiza Mhagama.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Nuru Ngeleja amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Nyasa kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo ambao amesema utachochea wananchi kukiamini Chama Tawala kuendelea kutawala.

Hata hivyo Ngeleja ameushauri uongozi wa Halmashauri ya Nyasa kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na serikali kuhakikisha  inatangazwa na kufahamika kwa wananchi ili kutambua kazi nzuri zinazofanywa na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu  ya CCM Taifa Musa Homera ameipongeza Kampuni ya SUMA JKT kwa kutekeleza mradi huo  ambapo amesema wananchi wa Nyasa wameonesha moyo wa kujitolea katika utekelezaji wa mradi huo.

“Naomba serikali iendelee kuwaamini zaidi SUMA JKT kutokana na kutekeleza vema miradi ambayo mnapewa ,wilaya ya Nyasa inafanya vizuri katika utekelezaji miradi,inagawa,imezipita wilaya nyingine kongwe katika Mkoa wa Ruvuma’’,alisisitiza Homera.

Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma inafanya ziara ya siku tano kupita katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma  kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.