Mahakama ya mjini Istanbul, Uturuki hii leo itasikiliza kesi dhidi ya raia 20 wa Saudi Arabia bila ya washtakiwa hao kuwepo mahakamani, baada ya kuhusishwa na mauaji ya mwandishi habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi mnamo mwaka 2018.
Mashtaka hayo yanamshutumu Ahmed al-Asiri, mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi ya Saudi Arabia, na Saud al-Qahtani, mshauri wa zamani mwanamfalme Mohammed bin Salman, kwa kuchochea mauaji yaliyopangwa kwa nia mbaya. Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia Arabia mjini Istanbul mnamo Oktoba 2, 2018.
Kulingana na hati ya mashtaka iliyoonekana na shirika la habari la dpa, Khashoggi alinyongwa hadi kufa na mwili wake ulikatwa vipande vipande. Mwendesha mashtaka anadai kifungo cha maisha kwa washtakiwa wote, ambayo ni adhabu kali zaidi kutolewa Uturuki tangu kukomeshwa hukumu ya kifo mnamo mwaka 2002.
