Rais wa Brazil apimwa virusi vya corona


Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiipuuza miongozo ya kujikinga na virusi vya corona amepimwa virusi hivyo baada ya kuonesha dalili ikiwemo kupata homa.

 Rais Bolsonaro ambaye mara kwa mara amekuwa akikataa kuvaa barakoa amesema pia amechunguzwa mapafu kwa kutumia kipimo cha picha cha X-ray katika hospitali ya kijeshi kama tahadhari.

''Ninaepuka kuwakaribia watu, kwa sababu nimetoka hospitali kupima COVID-19, lakini najisikia vizuri. Asilimia 90 ya watu watakaoambukizwa hawatokuwa na dalili. Tunachopaswa kufanya ni kutovieneza virusi kwa wengine. Iwapo nitaathirika virusi vya corona, sitokuwa na wasiwasi, itakuwa ni sawa kama kuwa na mafua au homa. Tuheshimu miongozo ya Wizara ya Afya,'' alifafanua Bolsonaro.


Majibu ya vipimo vya Bolsonaro yanatarajiwa kutolewa leo mchana. Rais huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 65, amesema amekuwa akitumia dawa ya hydroxychloroquine, kama hatua za kujikinga. Vyombo vya habari vya Brazil vimetangaza kuwa Bolsonaro amebadili ratiba yake ya wiki nzima, ingawa wasaidizi wake hawajatoa taarifa yoyote. Brazil ina zaidi ya wagonjwa 1,623,200 wa COVID-19 na zaidi ya watu 65,000 wamekufa kutokana na virusi hivyo.

Ama kwa upande mwingine, Chuo Kikuu cha Johns Hopkins kimetangaza kuwa idadi jumla ya watu walioambukizwa COVID-19 nchini Marekani imefikia 2,931,142 huku vifo vikiwa 130,248. Siku ya Jumatatu Marekani ilitangaza vifo vipya 357 na maambukizi 54,999.

Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya Ujerumani ya Robert Koch imesema kuwa idadi ya visa vya virusi vya corona nchini Ujerumani imeongezeka kwa 309 na hivyo kuifanya idadi jumla ya maambukizi kuwa 196,944. Taasisi hiyo pia siku ya Jumanneimerekodivifo vipya vinane na kuifanya idadi ya watu waliokufa kufikia 9,024.

Wizara ya afya ya China nayo imetangaza visa vipya vinane vya virusi vya corona. Maambukizi hayo ni ya wasafiri walioingia China kutoka nchi za nje. Hata hivyo hakuna vifo vyovyote. Hadi siku ya Jumatatu China ilikuwa na visa 83,565 vya virusi vya corona na vifo 4,634.

Mexico imerekodi visa vipya 4,902 na vifo 480 vya virusi vya corona. Idadi jumla ya maambukizi nchini Mexico imefikia 261,750 na vifo 31,119. Serikali imesema idadi kamili ya maambukizi huenda ikawa juu zaidi kuliko inayorekodiwa.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameonya kuwa janga la COVID-19 linaweza kutoa fursa mpya kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, mtandao wa kigaidi wa al-Qaida pamoja na washirika wao.

Hayo yanajiri wakati ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameonya kuwa janga la COVID-19 linaweza kuyanufaisha makundi ya wanamgambo.


Guterres pia ameonya kwamba makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia, wafuasi wa sera za Unazi mamboleo, makundi yanayodhani Wazungu ni bora zaidi ya wengine na makundi yanayoeneza chuki yanaweza kufaidika na janga hili.

Amesema ingawa bado ni mapema kutathmini athari ya ugaidi ilivyo kutokana na janga la virusi vya corona, makundi yote hayo yanajaribu kuleta mgawanyiko na kuutumia kusababisha migogoro, utawala mbovu na machungu waliyo nayo watu ili kuendeleza malengo yao ya wakati huu wa janga la COVID-19. Guterres amesema IS inajaribu kujipanga tena kuendesha operesheni Syria na Iraq, ambako iliwahi kudhibiti maeneo makubwa.

Benki ya Dunia na IMF kujadiliana kupitia mtandao

Aidha, mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF utafanyika mwezi Oktoba kwa njia ya mtandao kutokana na janga la virusi vya corona.

Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass amesema janga la COVID-19 na kuporomoka kwa uchumi kunatishia kurudisha nyuma maendeleo yaliyofikiwa katika miaka ya hivi karibuni na kuwarejesha mamilioni ya watu kwenye umasikini.

Amesema Benki ya Dunia imeidhinisha miradi ya dharura ya afya kwa zaidi ya nchi 100 na inatoa mitaji ya biashara kwa sekta binafsi kwenye nchi zinazoendelea.