Shirika la ndege la Pakistan lapigwa marufuku kuruka anga ya Ulaya


Shirika la usalama wa anga la Umoja wa Ulaya EASA, limelizuia shirika la ndege la kimataifa la Pakistan PIA, kuruka katika anga ya Ulaya kwa kipindi cha miezi sita.

Uamuzi huo umechukuliwa, baada ya wiki iliyopita wizara ya uchukuzi ya Pakistan kubaini marubani 262 kati ya 800, walikuwa na leseni bandia au walidanganya katika mitihani.

Nusu ya marubani hao walikuwa wafanyakazi wa shirika la ndege la PIA.

Shirika la anga la Ulaya limesema pamoja na tatizo la marubani lakini pia wana wasiwasi juu ya uwezo wa Pakistan wa kufuata kanuni za kimataifa za usalama wa anga wakati wote.

Miezi kadhaa iliyopita, shirika la PIA limeendesha safari chache za ndege kutokana na janga la kirusi cha corona. Lakini mara baada ya kurejsha huduma zake, ndege moja ilipata ajali na kuua watu 98.