TAKUKURU yajipanga kesi feki rushwa ya ngono


Na James Timber, Mwanza

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imesema imejipanga kikamirifu kufanya uchunguzi wa kesi zote za rushwa ya ngono zitakazoripotiwa na wanavyuo ili kuepuka kuwatia hatiani watu ambao watakaokuwa wamesingiziwa kujihusisha na vitendo hivyo.

Hayo yalisemw na Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Daud Ndyamukama wakati akifungua semina ya kupinga rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Chuo Cha Afya Bugando (BMC) pamoja na Chuo Cha Ualimu Butimba.

Ndyamukama alisema kutokana na kampeni ya kupinga rushwa ya ngono inayoendelea hivi sasa kwenye vyuo vyote nchi nzima chini ya usimamizi wa Takukuru  inawezekana kuna baadhi ya watu wenye roho ya visasi wanaweza tumia mwanya huo kufanya udanganyifu ili kuwatia hatiani watu wasio na hatia kwa kulitambua hilo taasisi hiyo imejiandaa kikamirifu kukabiliana na kesi kama hizo.

Alisema ni lazima jamii ya wanavyuo wote watambue kampeni ya kupinga rushwa ya ngono inayoendelea nchi nzima inafanyika kwa mjibu wa sheria ya Takukuru namba 11  ya mwaka 2007 hivyo kabla ya watuhumiwa kufikishwa mbele ya vyombo vya dora uchunguzi utafanyika kwa weledi ili kuepuka kuwatia hatiani watu waliosingiziwa.

Aidha Nyamukama aliongeza a kampeni hiyo kufanyika vyuoni haina maana kuwa jamii nyingine haiwahusu bali inafanyika kwenye taasisi hizo kutokana na  kuwa ndio wahanga wakubwa wa rushwa ya ngono na kupitia wanavyuo takukuru  inaamini inandaa mabalozi wazuri wa kupinga rushwa ya ngono hata watakapoingia kwenye soko la ajira serikalini ama kwa makampuni binafsi.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha SAUT, Daud Masanja alisema chuo hicho kilianza siku nyingi kuunga mkono vita ya rushwa ya ngono kwa kuanzia dawati la jinsia ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ambapo dawati hilo liliundwa kutoa misaada kwa wote watakaokumbana na changamoto za rushwa ya ngono.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia Chuo Kikuu SAUT, Sister Dk. Clara Rupia  alisema kupitia dawati hilo mwamuko wa wanafunzi kuunga mkono vita ya rushwa ya ngono umeonekana ni mkubwa kwani wale ambao wamekumabana na changamoto za kijinsia wamefika kwenye dawati hilo kupata ushauri ingawa hadi sasa hawajapokea kesi za rushwa ya ngono.

Awali akifungua mdahalo huo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Severine Ralika aliwataka washiriki kutoka vyuo vyote kulichukulia kwa uzito wake suala la rushwa ya ngono na kuzingatia kauli mbiu isemayo ‘vunja ukimya, kataa rushwa ya ngono’ ambapo aliwaomba kushiriki kutoa taarifa na mbinu za kukabiliana na tatizo hilo kwani limekuwa chanzo cha kuminya haki na hata kupelekea wanataaluma wasio na sifa.