Jimbo la Galicia lililoko kaskazini magharibi mwa Uhispania limeweka hatua mpya za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona kutokana na mripuko mpya wa virusi hivyo.
Uamuzi huo umechukuliwa siku moja baada ya jimbo la Catalonia kutangaza masharti yanayowazuia watu kutoka nje, ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
Aidha, serikali ya India imeamua kutolifungua tena eneo la kihistoria la Taj Mahal, kutokana na maambukizi kuongezeka kwa kasi kwenye mji wa Agra.
Naye rais mpya wa Malawi, Lazarus Chakwera amefuta maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo pamoja na sherehe za kuapishwa kwake kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya COVID-19.
Mexico jana imerekodi maambukizi mapya 4,683 ya virusi vya corona pamoja na vifo 273.
Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn ameonya kwamba virusi vya corona bado vipo, hivyo ni muhimu kuendelea kuvaa barakoa kila siku.
