Serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa yalaani mashambulizi Al-watiya


Serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imelaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa dhidi ya kambi muhimu ya jeshi la anga iliyokombolewa na wanajeshi wa serikali magharibi mwa nchi hiyo, ikidai yamefanywa na jeshi la nje.

Mwezi Mei, majeshi ya serikali ya mjini Tripoli, GNA yaliitwaa tena kambi ya jeshi la anga ya Al-Watiya, kusini magharibi mwa Tripoli kutoka kwa vikosi vya mashariki vinavyoongozwa na kamanda Khalifa Haftar.

 Naibu Waziri wa Ulinzi wa serikali ya GNA, Salah Namrush amesema mashambulizi hayo yaliyotokea usiku wa Jumamosi yamefanywa na kikosi cha anga cha kigeni bila ya kufafanua zaidi kuhusu kikosi hicho.

Awali, jeshi linaloongozwa na Haftar lilidai kuwa mashambulizi hayo yamefanywa na ndege zisizojulikana ambazo ziliulenga mtambo wa Uturuki wa kujikinga na makombora uliowekwa kwenye kambi ya Al-Watiya.