Kundi lijiitalo Dola la Kiislamu nchini Afghanistan limedai kuhusika na mashambulizi ya kujitoa muhanga na ya risasi katika gereza moja mashariki mwa nchi hiyo yaliyouwa watu watatu na kujeruhi wengine 24 hapo jana.
Hadi kufikia usiku wa kuamkia leo mapigano yalikuwa yakiendelea kati ya vikosi vya usalama na wapiganaji wa kundi hilo katika mji mkuu wa jimbo la Nangarhar, Jalalabad, ambapo idadi ya wahanga inahofiwa kuwa itaongezeka.
Mashambulizi yamefanyika siku moja tu baada ya shirika la ujasusi la Afghanistan kutangaza kuwa kamanda wa ngazi za juu wa kundi hilo aliuawa na vikosi maalum vya Afghanistan karibu na Jalalabad.
Msemaji wa Taliban, Suhail Shaheen, amelitenga kundi lake na mashambulizi hayo, akisema kwamba wanaheshimu tamko la kusitisha mapigano, kupisha sherehe za Eid Al Adh-ha zinazomalizika leo.
