Mvua kubwa iliyoambatana na mafuriko imesababisha vifo vya watu watano nchini Sudan huku nyumba zaidi ya 1,200 zikiharibiwa vibaya.
Taarifa kutoka jimbo la Blue Nile zinasema wanawake na watoto wanalala nje katika wakati ambapo watu zaidi ya 100,000 wameathiriwa vibaya na mvua na mafuriko hayo katika mji wa Bout. Shirika la Hilali Nyekundu limesema nyumba 120 zimeharibiwa kwenye mji mwengine wa jirani wa Wad Abuk.
Picha zilizosambazwa mitandaoni zinaonesha mikondo ya maji ikikata barabara na kuziporomosha nyumba na mali za watu.
Sehemu kubwa ya mashamba ya mazao yamefunikwa na maji. Mvua hiyo kubwa imesababisha pia kuvunjika kwa kingo za Bwawa la Bout na kuzifanya familia zaidi ya 600 kukwama zikiwa zimezungukwa na maji.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mvua kama hizi mwaka jana ziliuwa watu 18 katika majimbo 16 ya Sudan.
