Ramaphosa awaonya 'fisi' wanaoiba pesa za Covid-19


Rais wa Afria Kusini Cyril Ramaphosa ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu aliowaita ya "fisi " ambao wananufaika kutokana na pesa za umma ambazo zilipangiwa kutumiwa katika mapambano dhidi ya janga la virusi vya corona.

Kauli zake kali ambazo ziliandikwa katika waraka wake wa kila wiki, zinawalenga maafisa wa taifa hilo ambao wanashutumiwa kuchukua zabuni za serikali, wafanyabiashara ambao wanapandisha bei za usambazaji wa vifaa vya kinga (PPE), na maafisa utawala wa kimaeneo wanaojilimbikizia msaada wa chakula.

"Kujaribu kupata faida kutokana na janga ambalo linagarimu maisha ya watu wetu kila siku ni kitendo cha unyama. Nikama kundi la fisi waliozingira mzoga," alisema Ramaphosa.

Quote Message: Tunashuhudia wizi unaofanywa na watu binafsi na makampuni ambayo hayana hisia. from Cyril Ramaphosa Rais, Afrika Kusini
Tunashuhudia wizi unaofanywa na watu binafsi na makampuni ambayo hayana hisia.

Msemaji wake mwenyewe alichukua likizo wiki iliyopita baada mume wake kutajwa kuhusiana na zabuni katika idara ya afya ya jimbo la Gauteng. Yeye na mke wake walikanana kufanya kosa lolote.

Rais aliapa kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakaobainika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za Covid-19.

"Wale watakaopatikana na hatia ya kuvunja sharia kujitajirisha kupitia mzozo wataona cha mtemakuni , bila kujali ni akina nani au wana uhusiano na nani," alisema.

Afrika Kusini ndio nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi na mlipuko wa corona na idadi ya watu waliopatikana na virusi wamepita zaidi ya nusu milioni mwishoni mwa juma.