Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amekabidhi rasmi leo ofisi ya jiji hilo kwa Mkuu mpya wa mkoa wa mkoa Aboubakar Kunenge.
Bwana Makonda aliondolewa katika nafasi hiyo mwezi jana baada ya kugombea kiti cha ubunge wa jimbo la Kigamboni. Hata hivyo alishindwa katika kinyang'anyiro cha kura za maoni.
"Yote tuliyoyafanya unayajua na nina imani uwezo wa kuyasimamia unao kwa sababu tulifanya kazi pamoja. Ninamshukuru mheshimiwa rais (John Magufuli) kwa kukuchagua kuliongoza jiji hili", amesema Bwana Makonda ambaye anasema jambo ambalo anasikitika kuwa hakulitimiza alipokuwa madarakani ni kutoweza kufanikiwa kuanzisha upimaji wa tezi dume kwa kaya.
Bwana Makonda amewaambia Watanzania wasiwe na wawiwasi na maisha yake baada ya kuondoka katika kiti cha ukuu wa mkoa:
Quote Message: Muwe na wasiwasi mkisikia Makonda amemuacha Yesu , lakini kama sijamuacha Yesu msiwe na wasiwasi from Paul Makonda Mkuu wa Mkoa wa zamani Dar es Salaam
Muwe na wasiwasi mkisikia Makonda amemuacha Yesu , lakini kama sijamuacha Yesu msiwe na wasiwasi
"Mwendo nimeumaliza...Ninashukuru kwa kupata nafasi ya kutunza familia kama baba wa familia’’, amesema Makonda.
Akiwa madarakani, Makonda amevuta wafuasi na 'maadui' pia. Amekuwa akisifiwa kwa kuja na mipango kadhaa ya kusaidia jamii katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii.
Hata hivyo mipango hiyo pia imekuwa ikikosolewa kwa kutofuata taratibu rasmi na mwisho wa kueleweka.
Makonda pia alikosolewa kitaifa na kimataifa kwa kuvamia kituo binafsi cha habari Clouds Media Group na kutangaza vita dhidi ya wapenzi wa jinsia moja akiwa madarakani .
