Sudan yapongeza matamshi ya Pompeo kuhusu kuiondoa katika orodha ya ugaidi

Khartoum Serikali ya Sudan imekaribisha matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo wiki hii kwamba angependa kuiondoa Sudan katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi.

Haya ni kwa mujibu wa shirika la habari la serikali SUNA. Mara kwa mara Pompeo amekuwa akiashiria kwamba wizara hiyo inatarajia kuondoa sifa hiyo ambayo inaathiri vibaya uwekezaji nchini humo lakini mzozo umeibuka kuhusiana na kiwango cha fidia cha mashambulizi ya mabomu dhidi ya balozi mbili za Marekani mnamo mwaka 1998.

Siku ya Alhamisi, Pompeo aliiambia kamati ya bunge la seneti kuhusu uhusiano wa kigeni kwamba sheria kuhusu fidia inapaswa kuwasilishwa mbele ya bunge hivi karibuni. Shirika la habari la Sudan SUNA limeripoti kuwa serikali ya nchi hiyo jana iliahidi kufanya kila iwezavyo kuafikia matakwa yatakayoisaidia Marekani kuchukuwa hatua bora.

Aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al Bashir alikuwa amemkaribisha kiongozi wa kundi la Al- Qaeda Osama bin Laden na Sudan ikashtumiwa kwa kuyasaidia makundi ya itikadi kali yaliozishambulia balozi mbili za Marekani nchini Kenya na Tanzania na kusababisha vifo vya watu 224 na kujeruhiwa kwa wengine elfu 5.