Zaidi ya vyama 25 vya upinzani nchini Venezuela vimesema kwamba havitashiriki uchaguzi wa bunge unaofanyika Disemba mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na chama kikuu cha upinzani cha Voluntad Popular cha Juan Guaido hivi leo imesema vyama 27 vimesaini tamko la pamoja kutoshiriki kile walichosema ni "udanganyifu wa utawala wa kidikteta."
Baraza Kuu la Uchaguzi ambalo linaelemea upande wa Rais Nicolas Maduro lilitangaza mwezi uliopita kwamba uchaguzi wa bunge utafanyika tarehe 5 Disemba, lakini Guaido, mpinzani mkuu wa Maduro na ambaye baadhi ya mataifa yaliwahi kumtambua kama rais halali wa Venezuela, ameuita uchaguzi huo kuwa ni "kituko".
Maduro alishinda muhula wa pili katika uchaguzi wa Mei 2018 ambao pia ulisusiwa na wapinzani wake.
