Wafungwa wengi watoroka jela lililoshambuliwa Afghanistan



Kumetokea mapambano ya ufyatulianaji risasi kati ya wapiganaji wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS na vikosi vya usalama vya Afghanistan katika jela moja lililoko katika mji wa mashariki wa Jalalabad leo.

Karibu watu 24 wameuawa katika mapigano hayo baada ya wanamgambo hao wa IS kulivamia jela hilo usiku wa kuamkia leo na kusababisha idadi kubwa ya wafungwa kutoroka.

Shambulizi hilo lilianza jana jioni huku bomu lililotegwa ndani ya gari likilipuliwa katika lango kuu la jela hiyo. Adil Khan alishuhudia shambulizi hilo.

"Mara baada ya mlipuko wa kwanza, niliona watu wengi chini wamejeruhiwa. Nilijaribu kuondoka kwa kuwa sikuweza kusaidia yeyote aliyekuwa amejeruhiwa kwasababu milipuko ilikuwa inaendelea ila nashkuru Mungu maafisa wa usalama waliwasili."

Kulikuwa na milipuko mingine mingi iliyosikika wakati magaidi hao walipowafyatulia risasi walinzi. Kulingana na mbunge katika mkoa wa Nangarhar Sohrab Qaderi wanamgambo 30 ndio waliohusika katika shambulizi hilo katika jela lililokuwa na wafungwa 2,000.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Attaulah Khugyani, wanamgambo watatu waliuwawa katika shambulizi la awali huku takribani raia 21 na walinzi wa usalama wakifariki katika mapigano hayo. Watu 43 walijeruhiwa.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items