Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Katika kusherekea siku ya wazee Duniani ambayo huadhimishwa Octoba mosi kila mwaka Benki ya Posta Tanzania imeadhimisha siku hiyo kwa kutoa huduma za Afya bure na kukata keki pamoja na wazee ambao ni wateja wa benki hiyo.
Akizungumza mara baada ya tukio hilo Meneja wa Benki hiyo tawi la Dodoma bw. Shaban Telatela amesema wameamua kufanya tukio hilo baada ya kutambua mchango mkubwa unaofanywa na wazee ambao ni wateja wao wakubwa.
"Wazee ni wateja wetu wakubwa ni wazee hivyo leo katika kuadhimisha siku hii tumeona tuhudumie wateja wetu hawa kwa kuwaletea huduma za afya bure kabisa na kukata keki pamoja" amesema Telatela.
Amesema wazee wengi waliachwa nyuma hasa baada ya kustaafu lakini baada ya benki hii kuanzishwa tulitambua mchango wao na kuwapa mikopo ya kuboresha maisha yao baada ya kustaafu ili waishi kwa furaha.
Amesema benki inatambua kazi kubwa iliyofanywa na wazee katika kulitumikia taifa letu hivyo tukaamua kuanzisha mikopo hiyo ili kuboresha maisha ya wazee na hasa mikopo ya kuboresha makazi yao ili waishi kwa furaha.
" Zamani mzee alikuwa akistaafu walikuwa hawakopesheki lakini benki yetu ikaja na hii mikopo ambayo inasaidia Sana wazee kwanza kuboresha makazi yao na kujiendeleza kimaisha" amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wazee walioshiriki tukio hilo akiwamo bi Merry Lemanya, mkazi wa Hombolo Dodoma amesema katika huduma aliyoipata leo imemsaidia kujua hali yake ya afya kitu ambacho kitamsaidia katika kuimarisha afya yao.
Amesema benki hiyo imemsaidia sana hasa katika mikopo wanayopewa wazee hao imewasaidia Sana hasa katika kuboresha makazi yao na kujiendesha kimaisha katika miradi mbalimbali wanayoifanya kujiendesha kimaisha.

